AHADI YA VIONGOZI WA MILA (MALAWAGWANANI) KWA MKUU WA WILAYA YA LONGIDO KUHUSU KUTOA ELIMU NA HAMASA KWA JAMII YA WAFUGAJI KUHUSU KUJIANDIKISHA KWENYE ORODHA YA MPIGA KURA YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2024.
Viongozi wa mila (Malawagwanani) wilayani Longido wameahidi kutoa elimu na hamasa kwa jamii ya wafugaji katika jitihada za kuhakikisha ushiriki wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024. Ahadi hii ilitolewa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe.Salum Kalli, alipokutana na viongozi hao kujadili mikakati ya kuhamasisha jamii ya wafugaji kujisajili kwenye orodha ya wapiga kura.
Katika mkutano huo, viongozi wa mila walieleza dhamira yao ya kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kujiandikisha na kushiriki kwenye uchaguzi, wakisema kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia na kuhakikisha kuwa jamii yao inapata uwakilishi sahihi.Aidha viongozi hao Waliahidi kutumia mamlaka yao ya kijamii kushawishi na kuwahimiza wafugaji kuchukua jukumu la kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa tarehe 27 octoba 2024 kwa kuanza na hatua ya kujiandikisha.
Zoezi la uhamasishaji litaanza rasmi mara tu wataporejea kwenye maeneo yao ya utawala , na tayari viongozi hao wamekwishaanza kuhamasisha jamii kushiriki zoezi hilo muhimu. Malaigwanani hao Wamesema kuwa watapita kwa jamii na kwenye maeneo mbalimbali ili kufikisha ujumbe huu kwa wafugaji kwa njia zinazoeleweka na kuendana na maisha yao ya kila siku.
Mwenyekiti wa Malawagwanani wilaya, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutambua mchango wao katika jamii na kuahidi kumpa ushirikiano wa dhati katika kukamilisha zoezi hilo ili lifanikiwe kwa asilimia mia moja. Aliongeza kuwa viongozi wa mila wataendelea kushirikiana na serikali kwa ukaribu katika kuhakikisha kila mfugaji anapata nafasi ya kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi huo muhimu kwa maendeleo ya wilaya ya Longido.
Mkuu wa Wilaya ya Longido alitoa shukrani zake kwa viongozi hao kwa kuonyesha nia ya dhati ya kushirikiana na serikali katika kuhamasisha jamii. Alisisitiza kuwa ushiriki wa jamii ya wafugaji ni muhimu kwa maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla, na uchaguzi wa serikali za mitaa ni fursa nzuri ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya maendeleo ya eneo lake.
Kupitia ushirikiano huo, viongozi wa mila na serikali ya wilaya ya Longido wanaamini kuwa watafanikiwa kuongeza idadi ya wafugaji watakaojiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura, hivyo kuwezesha ushiriki wao kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM