Mkuu wa Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha Mhe. Nurudin Babu amekutana na kufanya majadiliano na viongozi wa Mila( Alaigwanani) pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali (dini) juu ya kuhakikisha wananchi wilayani hapa wanapata chanjo ya UVIKO 19.
Alisema Kumekuwa na baadhi ya wawakilishi wa wananchi kupotosha jamii dhidi ya chanjo inayoendelea kutolewa ya Johnson and Johnson (JANSSEN) na kupelekea wananchi kuingiwa na hofu na kukata kuchanja.
" Hakuna serikali duniani ipo kwa ajili ya kuua wananchi wake,na hata hapa kwetu Tanzania hakuna Kiongozi Yupo tayari kuua wananchi wake hivyo achaneni na Maneno ya wapotoshaji" alisema
Aidha alitoa angalizo kwa baadhi ya viongozi wenye tabia hiyo kuacha Mara moja kwani atawachukulia hatua Kali za kisheria ,huku akitoa agizo kwa wakuu wa idara ya elimu na afya kuhakikisha watumishi wote wa idara hizo wanapata chanjo ili kuwalinda watu na wanafunzi wanaowahudumia au kuwafundisha.
Naye Kaimu Mkurugenzi Ndugu Edward Mboya alimuhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa atahakikisha maagizo yote aliyotoa yanatekelezwa kwa wakati kabda ya zoezi hili kuisha kwa kuwahimiza watumishi wote wanaotoa huduma kwa jamii wanafuata taratibu zote za kujikinga na ugonjwa wa Korona UVIKO-19 na kuhakikisha wanapata chanjo ya UVIKO-19 hasa walimu na wahudumu wa afya.
Baadi ya wazee wa Mila walitoa maoni yao na kuzungumzia sababu ya jamii kukataa au kuogopa kuchanja ni Maneno dhidi ya chanjo hiyo kuwa inapunguza nguvu za kiume lakini pia tatizo kubwa ni jamii kukosa elimu dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19.
Hata hivyo viongozi hao wa Mila waliazimia kwa pamoja kuwa sauti ya jamii katika kukubali na kupokea chanjo hiyo,huku wakikiri kuwa ugonjwa huo upo na umeua watu wengi Sana hata ndani ya jamii na kumuahidi Mkuu wa wilaya kuwa watasaidia kueneza elimu juu ya umuhimu wa kupata chanjo kwenye jamii wanazotoka.
Kwa upande wao viongozi wa dini walisema watatoa elimu katika nyumba za ibada na kukemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa dini wanaopotosha wananchi juu ya chanjo na kusema masuala yanayohusiana na afya waachiwe wataalamu wa afya wao wabaki na mambo ya kiimani.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt Seleman Mtenjela alisema chanjo hiyo ni salama na wamefanikiwa kuchanja watu 867 sawa na asilimia 33 ya dozi iliyotolewa wilayani hapo,hata hivyo Kati ya hao waliopata chanjo hakuna aliyewahi kutoa taarifa Kama amepata madhara au kuwepo kwa taarifa za vifo.
" Maudhi madogo madogo yapo lakini ni ya kawaida kutokana na kitu kipya kinavyoingia mwilini, ikiwemo maumivu kiasi katika sehemu uliyochomwa sindano,uchovu,homa au baridi na maumivu ya kichwa" alisema.
Baadhi ya wananchi waliochoma chanjo hiyo wamekanusha uvumi kuhusu kupotea kwa nguvu za kiume na kusema wapo imara ,huku wengine wakisema hawajapata madhara yoyote ya kiafya.
Mwisho.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM