Na.HAPPINESS NSELU
Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Longido kwa kushirikiana na Shirika la Compassion linalotoa huduma za malezi kwa watoto na vijana kupitia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Namanga, wameendelea kutoa elimu kwa watoto wa kike ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 11.
Tukio hilo limefanyika Oktoba 13 katika kituo cha Compassion kilichopo Namanga, chini ya uratibu wa Mratibu wa kituo hicho, Elihuruma Pendael, likihusisha wasichana kutoka maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Bi Monica Wambura, Bi Elmina Thadei na Bi Scolastica Kimario ndio waliongoza utoaji wa elimu hiyo kwa kushirikiana na timu ya Shirika la Compassion, wakilenga kumjengea mtoto wa kike uelewa wa haki zake za msingi, ujasiri wa kujilinda dhidi ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa elimu katika kutimiza malengo yao ya maisha.
Aidha, wasichana walioshiriki walipewa taulo za kike kama sehemu ya kampeni ya kuwasaidia kutunza afya ya uzazi na kuondoa changamoto zinazoweza kuwazuia kuhudhuria masomo kwa ufanisi.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Mimi ni Msichana, Kinara wa Mabadiliko kwa Tanzania Tuitakayo 2050”, ikisisitiza jukumu la jamii katika kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu bora, ulinzi na fursa sawa za maendeleo.
Akizungumza katika tukio hilo, Bi Monica Wambura alisema elimu kwa mtoto wa kike ni msingi wa ustawi wa taifa, hivyo jamii inapaswa kumpa nafasi ya kujifunza, kujitambua na kutimiza ndoto zake bila vizuizi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Compassion Namanga, Elihuruma Pendael, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika jitihada za kumlinda na kumjengea mtoto wa kike uwezo kupitia elimu na malezi chanya, ili kufikia Tanzania yenye usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2050
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.