NA ABRAHAM NTAMBARA
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, leo Januari 7, 2026 ameanza ziara ya kata kwa kata yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wilayani humo, ambapo ameanzia katika Kijiji cha Eworendeke, Kata ya Kimokouwa.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Mhe. Kalli amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua ili kuchochea ustawi wa maendeleo katika maeneo yao.
“Tumekuja kusikiliza kero zenu na kuzitatua. Lengo ni kuona namna mtakavyopata ustawi wa maendeleo katika maeneo yenu. Huu ni mwendelezo wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba sisi, wasaidizi wake, tutoke maofisini na kuja kuwasikiliza wananchi,” amesema Mhe. Kalli.
Mhe. Kalli ameeleza kuwa atafanya ziara katika kata zote 20 za Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Aidha, katika ziara hiyo, DC Kalli amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Longido kuchangamkia fursa ya Bima ya Afya kwa Wote kwa kuhakikisha wanajiunga na bima hiyo itakayowawezesha kupata huduma za afya kwa urahisi mahali popote nchini.
Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kampeni aliahidi kuhakikisha kuwa ifikapo siku 100 tangu kuanza kwa awamu ya pili ya uongozi wake, kuanzia Novemba 3, 2025 alipoapishwa, kila Mtanzania anakuwa na Bima ya Afya.
Katika mwendelezo wa ziara hiyo, kesho Januari 8, 2026, Mhe. Kalli anatarajiwa kuendelea na ziara yake katika Kata ya Sinonik.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: +255 272 970 793/ 94
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.