Na Happiness Nselu
Halmashauri ya Wilaya ya Longido imeadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji tarehe 7 Agosti 2025 kwa mafanikio makubwa kupitia sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Eorendeke, Kata ya Kimokouwa, na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, watoa huduma za afya na viongozi wa jamii.
Maadhimisho hayo, yaliyolenga kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto wachanga na lishe bora kwa familia, yalipambwa na uwepo wa Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Salumu Kalli, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Methew Majani, akisoma risala rasmi, alieleza dhamira ya halmashauri katika kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto. Alisisitiza kuwa unyonyeshaji sahihi unalinda afya ya watoto wachanga, unapunguza vifo vya watoto na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Afisa Lishe wa Wilaya, Bi Adelina Kahija, alitoa elimu kwa kina kwa kina mama na walezi kuhusu umuhimu wa kunyonyesha ndani ya saa moja baada ya kujifungua, unyonyeshaji wa pekee kwa miezi sita ya mwanzo, na kuhakikisha familia inapata mlo kamili wenye virutubisho muhimu.
“Tunataka kila kaya hapa Longido ifahamu kuwa unyonyeshaji ni msingi wa kizazi chenye afya, na lishe bora ni jukumu la familia nzima,” alisema, akihimiza wanaume kushirikiana na wake zao katika jukumu hilo.
Sherehe hizo zilipambwa na burudani kutoka kikundi cha muziki cha ACE Group, kilichotumbuiza kwa nyimbo zenye ujumbe wa kuhamasisha unyonyeshaji, malezi bora ya mama na mtoto, pamoja na ulaji wa chakula chenye virutubisho.
Mheshimiwa Kalli alisifu waandaaji na wadau kwa jitihada zao, akiwataka wananchi kuyatumia mafunzo yaliyotolewa. “Mama mwenye afya analea mtoto mwenye afya, na mtoto mwenye afya anajenga taifa imara,” alisisitiza.
Wiki ya Unyonyeshaji huadhimishwa duniani kote kila mwaka katika wiki ya kwanza ya Agosti, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema "THAMINI UNYONYESHAJI ;WEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA MAMA NA MTOTO".
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.