Na Happiness E Nselu
Katika juhudi za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido imekabidhi pikipiki nne kwa maafisa wa Idara ya Afya na Maendeleo ya Jamii. Hatua hii inalenga kurahisisha utendaji kazi wa maafisa hao kwa kuwafikia wananchi walioko maeneo ya vijijini, hususan maeneo yenye changamoto za kijiografia.
Akikabidhi pikipiki hizo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Salumu Kalli, aliishukuru ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa kujali mahitaji ya idara hizo na kuonyesha dhamira ya kuimarisha huduma kwa wananchi. Aidha, Mheshimiwa Kalli alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha sekta za afya na maendeleo ya jamii, ambazo zimewezesha upatikanaji wa nyenzo hizo muhimu.
Mheshimiwa Kalli aliwataka maafisa waliopokea pikipiki hizo kuhakikisha wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, akisisitiza kwamba hazipaswi kutumika kwa shughuli binafsi kama vile bodaboda au biashara nyingine. "Pikipiki hizi ni kwa ajili ya wananchi. Tutawafuatilia kuhakikisha zinatumika ipasavyo katika kutoa huduma bora kwa jamii," alisema.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Grace Mghase, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya, alisema kuwa pikipiki hizo ni sehemu ya jitihada za halmashauri ya kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa haraka. “Nyenzo hizi zitatusaidia kufanikisha malengo yetu ya kuwafikia wananchi hata katika maeneo yaliyo mbali,” alisema Bi. Mghase.
Afisa Afya wa Wilaya, Bi. Judithi Meela, alitoa shukrani kwa ofisi ya mkurugenzi kwa kuwezesha upatikanaji wa pikipiki hizo muhimu. Alisema kuwa pikipiki hizo zitakuwa mkombozi mkubwa kwa maafisa wa idara ya afya katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.
Naye Bw. Musa Kabula Afisa maendeleo ya jamii, aliyepokea pikipiki hizo kwa niaba ya maafisa wa Maendeleo ya Jamii, alisema kuwa nyenzo hizo zitawasaidia kufanikisha kazi zao katika maeneo yote ya wilaya. “Changamoto za miundombinu hazitakuwa tena kikwazo. Sasa tunaweza kuwahudumia wananchi wetu kwa wakati unaofaa,” alisema huku akitoa shukrani kwa uongozi wa halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Longido inaendelea kuonyesha dhamira yake ya kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kupitia uwekezaji wa rasilimali muhimu. Hatua kama hizi si tu zinaharakisha maendeleo ya kijamii bali pia zinaimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi wake.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM