Na. Happiness Nselu.
Wananchi wa Wilaya ya Longido wameandika historia mpya baada ya huduma za upasuaji kuanza rasmi katika Kituo cha Afya cha Eworendeke, hatua inayotarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za afya kwa wakazi wa maeneo ya vijiji na vitongoji vya karibu.
Mnamo Tarehe 29 /08/2025, upasuaji wa kwanza kwa mama mjamzito ulifanyika kwa mafanikio makubwa, ambapo mama na mtoto wote wameripotiwa kuwa salama. Hii imekuwa ni ishara ya mwanzo wa huduma endelevu za upasuaji ambazo zitapunguza vifo vitokanavyo na uzazi na dharura nyingine za kiafya.
Awali, wananchi wa Longido walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za upasuaji katika hospitali za miji jirani kama Hospitali ya Wilaya ya Longido, Hospitali ya Rufaa Mount Meru Arusha, jambo lililosababisha gharama kubwa na wakati mwingine kuhatarisha maisha kutokana na ucheleweshaji wa matibabu. Kupatikana kwa huduma hizi ndani ya wilaya ni suluhisho muhimu kwa wananchi na kielelezo cha dhamira ya serikali kuboresha afya kwa wote.
Ufanikishaji wa huduma hizi umetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali imewekeza katika miundombinu, vifaa tiba vya kisasa na rasilimali watu, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya karibu na makazi yake.
Aidha, shukrani maalum zinatolewa kwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya, RHMT (Timu ya Afya ya Mkoa wa Arusha) na CMT-Longido (Timu ya Uendeshaji wa Halmashauri) kwa miongozo na usimamizi madhubuti uliofanikisha kuanzishwa rasmi kwa huduma za upasuaji katika kituo hiki.
Kipekee, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro B. Shemzigwa, amepongezwa kwa kusimama bega kwa bega na watumishi wa sekta ya afya kuhakikisha malengo ya serikali katika sekta ya afya yanafikiwa. Jitihada zake pamoja na ushirikiano wa karibu na timu ya usimamizi wa huduma za afya wilayani (CHMT) zimekuwa chachu ya mafanikio haya.
“Huduma hizi za upasuaji ni ukombozi kwa wananchi wa Longido. Tunashukuru uongozi wa serikali na wadau wote waliochangia kuhakikisha leo hii historia mpya imeandikwa,” imesema sehemu ya taarifa rasmi ya Halmashauri.
Kwa kuanzishwa kwa huduma hizi, wananchi wa Longido na maeneo ya jirani watanufaika kwa:
Kupata huduma za upasuaji kwa haraka na karibu zaidi.
Kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama wajawazito.
Kuokoa gharama za usafiri na rufaa za mbali.
Kuongeza ufanisi wa huduma za afya kwa jamii ya wafugaji na wakulima wanaoishi maeneo ya pembezoni.
Wananchi wa Longido wametakiwa kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuunga mkono juhudi za uboreshaji wa sekta ya afya na kuhakikisha huduma hizi zinadumu. Pia, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutumia huduma zinazotolewa katika kituo cha afya cha Eworendeke na vituo vingine vya afya vilivyoboreshwa ndani ya wilaya.
Timu ya watumishi wa afya wa Longido, hususan CHMT na madaktari bingwa wa upasuaji, imepongezwa kwa kujitoa na kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha huduma hii inaanza kwa mafanikio. Pia, wadau mbalimbali wa maendeleo waliowezesha kupatikana kwa vifaa na msaada wa kitaalamu wametajwa kama nguzo muhimu katika safari hii.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.