Na Happiness Nselu
Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha leo Septemba 26, 2025 imeadhimisha Siku ya Wazee Duniani kwa kaulimbiu: “Wazee Kushiriki Katika Uchaguzi kwa Ustawi wa Jamii Yetu.” Maadhimisho hayo yamefanyika katika Ukumbi wa J.K. Nyerere, yakihudhuriwa na mamia ya wazee kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya na mkoa mzima.
Shughuli zilizofanyika katika maadhimisho haya ni nyingi na zenye manufaa, ikiwemo:
Upimaji wa Afya: vipimo vya shinikizo la damu, sukari, macho na hali ya lishe
Ugawaji wa miwani bure kwa wazee waliobainika kuhitaji
Burudani
Chakula na vinywaji vya pamoja ambavyo vilikamilisha furaha ya siku hiyo
Akizungumza wakati wa maadhimisho, Katibu Tawala Wilaya ya Longido, Bi. Rahma Kondo, alisema Serikali imedhamiria kutoa huduma bora na mikakati madhubuti ya kusaidia wazee, ikiwemo huduma za matibabu na kutatua changamoto za kijamii zinazowakabili.
“Wazee ni hazina ya taifa letu. Ni jukumu letu kama jamii kuendelea kuwatunza, kuwasikiliza na kuwatumia hekima yao katika maendeleo ya kijamii na kitaifa,” alisema Bi. Kondo.
Bi. Kondo pia aliwataka wazee kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, akisisitiza kuwa sauti zao zina mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa taifa na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wao, Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa Bw. Denis Mgiye, Afisa Ustawi Wilaya Bw.A bdalah Nyange pamoja na Mwenyekiti wa Wazee walitoa salamu kwa wazee, wakisisitiza mshikamano, heshima, na umuhimu wa kizazi kipya kujifunza kutoka kwa hekima na uzoefu wa wazee.
Wazee waliohudhuria walifurahia sana siku hiyo, wakicheza, kuimba, kula na kunywa pamoja na viongozi na wananchi. Wengi walieleza kuwa maadhimisho hayo yamewapa matumaini mapya na kuthibitisha kuwa bado wanathaminiwa na taifa.
Siku ya Wazee Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba 1 tangu ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1990. Lengo kuu ni kutambua mchango wa wazee katika jamii, kuhakikisha haki zao zinalindwa, na kuhamasisha ustawi wao wa kijamii, kiuchumi na kiafya. Tanzania imekuwa ikishiriki maadhimisho haya kila mwaka kwa kutoa huduma za kijamii na kiafya kwa wazee, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuthamini na kuenzi wazee.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.