Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, ameandaa bonanza la uchaguzi kwa lengo la kuhamasisha jamii na kuongeza uelewa kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024. Bonanza hili lilifanyika katika viwanja vya Halmashauri, vilivyopo karibu na Kituo cha Polisi Longido, ambapo timu za Longido Staff na Veteran FC zilipambana katika mchezo wa soka.
Katika mchezo huo, Veteran FC walionyesha umahiri wao na kuibuka na ushindi wa bao 2 kwa sifuri dhidi ya Longido Staff. Mchezo huu ulilenga kutoa fursa ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi, huku pia ukilenga kukuza umoja na mshikamano miongoni mwa vijana.
Akizungumza kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya, Bw. Nestory Dagharo, alisisitiza kuwa michezo ni njia bora ya kuhamasisha vijana kushiriki katika uchaguzi. Alisema, "Vijana ni nguvu ya Taifa, na Taifa linawategemea vijana ili liende mbele. Michezo ni njia bora ya kuhamasisha ushiriki wao katika shughuli za kijamii na uchaguzi wa serikali za mitaa."
Pia, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Bw. Elimeliki Ukwai, alitoa elimu kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka wananchi wa Wilaya ya Longido kutumia fursa ya uchaguzi wa tarehe 27 Novemba 2024 kwa kuelekea vituoni na kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa maendeleo ya vijiji, kata, tarafa, na wilaya kwa ujumla. Alisisitiza kwamba kila raia ana wajibu wa kushiriki katika uchaguzi huo ili kuhakikisha uongozi bora na maendeleo ya maeneo yao.
Vilevile, Mchezaji wa Longido Staff, Bw. Steven, alieleza kuwa mechi hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwao, kwani ilileta umoja na mshikamano miongoni mwa vijana, hasa wa Tanzania. Alisema kuwa mchezo huu umekumbusha vijana wajibu wao katika kutumikia taifa na kuleta mabadiliko chanya kupitia ushiriki wao katika shughuli za kijamii, ikiwa ni pamoja na uchaguzi.
Bonanza hili limekuwa ni jukwaa muhimu kwa kuhamasisha wananchi, na hasa vijana, kutambua haki na wajibu wao katika michakato ya kisiasa na kijamii, ikiwa ni sehemu ya kujenga taifa lenye nguvu na umoja.
"SERIKALI ZA MITAA SAUTI YA WANANCHI JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI".
LONGIDO TUTASHIRIKI 27 NOVEMBA 2024.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM