Na Happiness Nselu
Halmashauri ya Wilaya ya Longido imepokea tuzo ya pongezi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI baada ya kufanikisha lengo la ufaulu lililowekwa kwenye Key Performance Indicator (KPI) katika Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili kwa mwaka 2024.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa mara ya kwanza wakati wa mkutano wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika katika Manispaa ya Iringa, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI – Elimu, Ndg. Atupele W. Mwambene, aliipongeza Halmashauri ya Longido kwa mafanikio hayo ya kitaaluma.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndg. Mwambene alisema kuwa Longido imeonyesha mfano wa kuigwa katika kusimamia taaluma, kuwajengea walimu mazingira bora ya kufundisha na kushirikisha jamii katika maendeleo ya elimu.
“Tumeona matokeo ya juhudi zenu. Longido ni miongoni mwa halmashauri zilizofikia viwango vya ufaulu tulivyovitarajia. Hili ni jambo la kujivunia,” alisema.
Mara baada ya kuwasili Longido, tuzo hiyo imekabidhiwa rasmi leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro Shemzigwa, ambaye alipokea kwa niaba ya timu nzima ya elimu ya halmashauri hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bw. Shemzigwa ameishukuru TAMISEMI kwa kutambua juhudi za halmashauri yake, na kusema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano, nidhamu ya kazi na usimamizi mzuri wa walimu pamoja na viongozi wa elimu katika ngazi zote.
“Tuzo hii ni motisha kubwa kwetu. Itaendelea kutusukuma kufanya vizuri zaidi, si tu kwa Kidato cha Pili, bali katika nyanja zote za elimu,” alisema Shemzigwa.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka TAMISEMI, Longido imepanda kwa kasi katika viwango vya ufaulu ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo linaloashiria ufanisi wa mikakati ya kuinua kiwango cha elimu vijijini.
Hii ni mara ya kwanza kwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kutunukiwa tuzo ya aina hiyo, hatua inayoweka historia mpya na kuongeza hamasa kwa wadau wa elimu wilayani humo.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM