Na Happiness Nselu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bwana Nassoro Shamzigwa, amefanya mazungumzo na wadau wa sekta ya utalii wanaotekeleza shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kikao hicho, kilichofanyika Tarehe 12 Agosti 2025 katika ukumbi Mdogo wa Halamshauri ya Wilaya ya Longido, kililenga kujadili njia bora za kuendeleza na kutangaza vivutio vya kitalii na urithi wa utamaduni wa Longido, pamoja na kutatua changamoto zinazokabili wadau hao wa sekta ya utalii.
Bwana Shamzigwa alisisitiza umuhimu wa wadau kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda rasilimali za kitalii na kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa tija na endelevu.
“Tukizingatia sheria na kanuni, tutalinda urithi wetu wa kipekee, kuongeza wageni, na kukuza pato la wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Rajab Mmunda, aliwapongeza wadau hao kwa kuchagua Longido kama eneo la shughuli zao za kitalii, akibainisha kuwa mchango wao unaongeza mapato ya halmashauri na serikali. Aliahidi kwamba maoni na changamoto zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi ili kuboresha zaidi sekta hiyo.
Kwa upande wake, Bw. Ally Mwako, Mratibu wa Longido Cultural tourism, alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kuitisha kikao hicho, akisema kuwa hatua hiyo ni ishara ya dhamira ya serikali kushirikiana na wadau katika kukuza utalii na urithi wa utamaduni.
Bwana Mwako aliahidi kuwa wadau wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha sekta ya utalii inakua kwa mpangilio unaonufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.