SERIKALI inafanya mapitio na kufanya uchunguzi wa miradi yote ya maji nchini ili kubaini inayofanya kazi na isiyofanya kazi.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alitoa uhakika huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini, Menrad Kigola (CCM) aliyetaka kujua Serikali inafanyika nini kuboresha miradi ya maji iliyoanzishwa, lakini haifanyi kazi.
Alisema serikali inapitia miradi hiyo ikiwamo ya maji iliyojengwa Mufindi Kusini ambako matangi 11 yalijengwa, lakini hayana maji.
Naibu Waziri alisema mara uchunguzi huo utakapokamilika, mkakati wa Serikali utakuwa kuboresha miundombinu ya maji ikiwamo kusafisha matangi na visima vilivyochimbwa ambavyo havina maji ili kuhakikisha vinafanya kazi.
Akijibu swali la msingi la mbunge huyo aliyetaka kujua serikali itamaliza lini ujenzi wa mradi wa Maji Sawala, Mtwango, Lufuna na Kibao, Kamwelwe alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni mosi, 2015 na ulitarajiwa kukamilika Juni mosi, mwaka jana.
Alisema utekelezaji wa mradi huo ulipangwa kufanyika kwa awamu tatu ambazo ni kujenga mahali pa kutega maji na kupeleka maji katika kijiji cha Sawala.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji imefanyika katika kijiji cha Sawala kwa gharama ya Sh milioni 644.21 na hadi sasa Sh milioni 261.64 zimetumika katika mradi huo.
Kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa mahali pa kuchukua maji, visima, boma za nyumbani na ulazaji wa bomba kuu, ujenzi wa tangi mita za ujazo 200 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 16 na ehemu ya mabomba ya usambazaji kilometa 3.4 kwa wastani wa kazi umefanyika kwa asilimia 50 kwa kijiji cha Sawala tu.
Mradi huo haukukamilika kwa wakati kutokana na mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba.
Novemba mwaka huu, halmashauri ya wilaya ya Mufindi ilivunja mkataba na mkandarasi huyo, na kuamua kutangaza upya Februari 7, mwaka huu ili kumpata mpya.
Mkandarasi anatarajiwa kupatikana Juni mwaka huu, na kazi itakamilika katika mwaka huu wa fedha.
Chanzo Habari Leo. By Joseph P Mkumbwa
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM