Na Happiness Nselu , Longido
Katika juhudi za serikali ya awamu ya sita kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuondokana na utegemezi wa nishati chafu kama kuni na mkaa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa mitungi 50 ya gesi kwa mama na baba lishe wa Wilaya ya Longido.
Zoezi la ugawaji wa mitungi hiyo limefanyika kwa mafanikio makubwa na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, ambaye alikabidhi rasmi mitungi hiyo kwa wajasiriamali hao wadogo kama sehemu ya mpango wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuboresha afya za wananchi.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mhe. Kalli alisema kuwa dhamira ya Rais ni kuhakikisha kila kaya, hasa zinazojihusisha na shughuli za upishi, zinatumia nishati safi ili kuokoa mazingira na kupunguza athari za kiafya zitokanazo na moshi wa kuni na mkaa.
“Rais amedhamiria kuona Watanzania wanapika kwa usalama zaidi na kwa njia ya kisasa. Mitungi hii ya gesi si tu kwamba itarahisisha kazi zenu, bali pia ni mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira,” alisema Mhe. Kalli.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo, Bi Grace Mghase, alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakazi wa Longido kuunga mkono juhudi za serikali kwa kubadilika kifikra na kuachana na matumizi ya nishati chafu.
“Hii ni fursa muhimu kwa jamii yetu. Tukiendelea kutumia kuni na mkaa, tunaharibu misitu na afya zetu pia ziko hatarini. Gesi ni njia salama, safi na ya haraka katika shughuli za kila siku, hasa kwa mama na baba lishe ambao muda ni rasilimali muhimu,” alieleza Bi Mghase.
Kwa upande wake, mama Saruni ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mama na Baba Lishe wilayani humo, alitoa shukrani kwa serikali kwa kuwakumbuka wafanyabiashara wadogo na kuwapatia vifaa vinavyowawezesha kuboresha huduma zao kwa wateja.
“Kwa kweli tumefurahi sana. Hatua hii ni ya kihistoria kwa sisi mama na baba lishe wa Longido. Tunaahidi kuzitumia mitungi hii kwa uangalifu, tukiwa na lengo la kuboresha huduma zetu na kuhakikisha wateja wetu wanapata vyakula bora kwa wakati,” alisema mama Saruni kwa furaha.
Wananchi waliohudhuria tukio hilo walionekana wenye hamasa kubwa huku wengi wakisema kuwa hatua hiyo imewapa mwanga kuhusu umuhimu wa kuhama kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa kwenda kwenye nishati safi kama gesi, jua, na umeme wa uhakika.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Jamii, mpango wa ugawaji wa nishati safi utaendelea kutekelezwa kwa awamu mbalimbali, huku vikundi vya wajasiriamali, mashule, na taasisi za kijamii vikipewa kipaumbele katika mgao wa vifaa hivyo.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM