Na. Happiness Nselu - Longido
Longido, Septemba 9, 2025 – Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro B. Shemzigwa, amewatakia kila laheri wanafunzi wote wa darasa la saba wa wilaya hiyo pamoja na Tanzania kwa ujumla, akiwataka kufanya mitihani yao kwa amani, utulivu na nidhamu.
Kwa mujibu wa takwimu za Halmashauri, jumla ya shule 63 wilayani Longido zinatarajia kushiriki katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu 2025. Idadi ya wanafunzi wote ni 3,218, kati yao wavulana 1,630 na wasichana 1,588.
Miongoni mwao, wapo wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye uoni hafifu na changamoto nyingine za kiafya, ambao pia wamepatiwa maandalizi ya kushiriki mitihani hiyo kwa usawa na wenzao.
Akizungumza leo ofisini kwake, Bw. Shemzigwa alisema: “Walimu na walezi wamefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kufanya vizuri. Ni matumaini yangu mitihani itafanyika kwa utulivu na amani, na matokeo yatakuwa mazuri yatakayowawezesha wanafunzi wetu kuendelea na elimu ya sekondari.”
Aidha, amesisitiza kuwa mitihani hiyo ni hatua muhimu kwa maisha ya kila mtoto, hivyo jamii kwa ujumla inapaswa kushirikiana kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki kwa wanafunzi wote katika kipindi hiki.
Mkurugenzi ameongeza kuwa mafanikio ya mitihani hiyo yanategemea mshikamano kati ya walimu, wazazi na jamii kwa ujumla. Alisisitiza kuwa malezi ya pamoja na ushirikiano wa karibu vitawasaidia watoto kushinda changamoto na kuongeza ari ya kujifunza.
Kwa upande mwingine, viongozi wa elimu wilayani Longido wamesisitiza kuwa maandalizi yamekamilika na shule zote zipo tayari kwa mitihani. Walimu wameendelea kuwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii, kujiamini na kudumisha nidhamu.
Halmashauri ya Wilaya ya Longido inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kuhakikisha kila mtoto, ikiwemo mwenye mahitaji maalumu, anapata nafasi sawa ya kushiriki mitihani hii muhimu. Lengo kuu ni kuhakikisha elimu bora na yenye usawa inapatikana kwa wote, sambamba na dira ya taifa ya maendeleo ya sekta ya elimu.
✍️ Idara ya Mawasiliano Serikalini – Halmashauri ya Wilaya ya Longido
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.