Na. Hppiness Nselu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ametoa maagizo kwa watendaji wa Wilaya ya Longido kuhakikisha wanawafikia wananchi katika maeneo yao na kushughulikia kwa haraka migogoro iliyopo, ili kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo, Septemba 4, 2025, katika ukumbi wa J. K. Nyerere wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, CPA Makalla alikutana na watumishi wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wa mila, ambapo alisisitiza kuwa migogoro mingi inayojitokeza katika jamii inaweza kumalizwa mapema iwapo watendaji wa serikali watafika kwa wananchi na kusikiliza changamoto zao.
“Watendaji lazima mjenge mazoea ya kuwafuata wananchi, msisubiri malalamiko yafike ofisini. Migogoro mingi ya ardhi na kijamii inaweza kumalizwa mapema ikiwa viongozi watashirikiana na wananchi kusikiliza na kutatua changamoto zao,” alisema CPA Makalla.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mila, Bw. Lekule Laizer, aliahidi kushirikiana kwa karibu na serikali na taasisi za usalama katika kuhakikisha migogoro inatatuliwa mapema na kwa njia za amani, ili wilaya iendelee kusonga mbele kimaendeleo.
Aidha, viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama walisisitiza kuwa wataendelea kutoa ushirikiano wa karibu na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika jamii zinashughulikiwa kwa wakati.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.