Na Happiness Nselu
Mkuu wa Wilaya ya Longido ameungana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Labani Kihongosi, pamoja na mamia ya wananchi wa Mkoa wa Arusha katika mazoezi ya viungo (Jogging) yaliyofanyika mapema jana kwenye Viwanja vya Mgambo, Uzunguni Jijini Arusha.
Jogging hiyo imekuwa sehemu ya ufunguzi wa Tamasha la Tanzania Samia Connect, lililoanzishwa na Mhe. Kihongosi kwa lengo la kusherehekea mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Longido alisema ushiriki wake pamoja na viongozi wengine ni ishara ya mshikamano na mshirikiano kati ya serikali na wananchi katika kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa nchini.
Mbali na maadhimisho, tamasha hilo linatoa huduma mbalimbali bure kwa wananchi, ikiwemo vipimo na matibabu ya macho, uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu. Zaidi ya miwani 3,000 zinatarajiwa kutolewa bure kwa wagonjwa watakaobainika kuhitaji.
Huduma nyingine zitakazopatikana kuanzia jana hadi kilele cha tamasha Agosti 23, 2025, ni pamoja na utoaji wa hati za ardhi, vitambulisho vya taifa na uraia, ukaguzi bure wa magari, pamoja na huduma zinazotolewa na mashirika ya serikali, taasisi na sekta binafsi.
Aidha, tamasha hilo limekuwa fursa kwa wajasiriamali wadogo kuuza bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula, hivyo kuongeza kipato na kujenga uchumi wa wananchi.
Kwa mujibu wa RC Kihongosi, Tanzania Samia Connect ni jukwaa la mshirikiano, linalolenga kuimarisha mshikamano kati ya wananchi na serikali sambamba na kusherehekea hatua kubwa za maendeleo zilizopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.