Na Happiness Nselu.
Shirika lisilo la kiserikali la MONDO Tanzania limekabidhi magodoro 32 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Longido, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono elimu jumuishi wilayani humo.
Makabidhiano yalifanyika shuleni Longido na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa MONDO na wadau wa maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa MONDO Tanzania, David Kereyani Kinisi, alisema msaada huo ni mwendelezo wa jitihada za shirika hilo katika kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwapatia vifaa kama magodoro, vitanda, mashine za kusomea kwa watoto wenye uoni hafifu na kuwawezesha kufika hospitalini kwa uchunguzi wa macho.
“Wapo watoto waliokuwa hawaoni kabisa, lakini baada ya uchunguzi na usafishaji wa macho, baadhi yao wameanza kuona kwa kiwango fulani,” alisema Kinisi.
Msaada huo ulipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Longido,Mhe. Salum Abdalah Kalli, ambaye aliishukuru MONDO TANZANIA kwa mchango wake wa kuboresha maisha ya watoto wenye changamoto.
Naye Mkuu wa shule hiyo,Mwl. Charles Mmbando, alisema magodoro hayo yataboresha mazingira ya kulala kwa wanafunzi na kuongeza ari ya kujifunza.
Bi. Tunu Manga, mmoja wa wadau wa maendeleo, alitoa wito kwa jamii kuwapeleka shule watoto wenye mahitaji maalumu badala ya kuwaficha, kwani kuna mashirika kama MONDO TANZANIA yanayotoa msaada.
Dada Mkuu wa shule hiyo alieleza kuwa msaada huo umewaletea faraja kubwa watoto waliokuwa wakilala katika mazingira duni.
MONDO TANZANIA imeendelea kuwa mshirika wa maendeleo ya elimu na huduma jumuishi kwa watoto wenye mahitaji maalumu Longido.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.