NA MWANDISHI WETU
Shirika la The Foundation for Tomorrow (TFFT) limewatambulisha rasmi wadau wa elimu mradi wake mpya wa kuimarisha ubora wa elimu ya msingi wilayani Longido. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi ya Elimu Msingi ya Halmashauri ya Wilaya.
Wajumbe wa TFFT walipokelewa na Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri, ambapo walieleza kuwa mradi unalenga kutoa mafunzo kwa walimu kuhusu KKK na lishe mashuleni. Mradi pia unajumuisha tuzo kwa walimu na shule zitakazofanya vizuri, ili kuhamasisha ubora wa elimu na maendeleo ya shule.
Meneja wa Programu ya Walimu wa TFFT, Amani Nicolas, aliwasilisha taarifa ya mradi na kueleza kuwa mojawapo ya malengo makuu ni kuongeza ushiriki wa wazazi na jamii katika maendeleo ya shule. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu kwa mafanikio ya elimu ya watoto.
Mkurugenzi wa Mradi, Noah Kayanda, alisema TFFT inalenga kushirikiana kwa karibu na walimu na Halmashauri ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, aliongeza kuwa masuala ya lishe mashuleni yatazingatiwa kama sehemu ya kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido aliipongeza TFFT kwa kuleta mradi unaolenga kushughulikia changamoto halisi za elimu na akahakikishia ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wake.
Mradi unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika shule mbalimbali za msingi wilayani Longido, ukiwa na lengo la kuleta mabadiliko chanya katika ubora wa elimu na ustawi wa wanafunzi.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: +255 272 970 793/ 94
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.