NA ABRAHAM NTAMBARA
Halmashauri ya Wilaya ya Longido imetoa mafunzo ya Mfumo wa Taarifa za Shule (SIS) kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, walimu wa mifumo pamoja na Maafisa Elimu Kata wilayani humo.
Mfumo wa SIS unaratibu usajili wa wanafunzi na walimu, pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya kitaaluma, mienendo ya tabia za walimu na motisha ya kitaaluma shuleni.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika kuanzia Januari 7, 2026 na kuhitimishwa leo Januari 8, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri wa J.K. Nyerere, Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Longido, Mwalimu Donat Bunonus, amewataka walimu hao kutumia mfumo huo kama nyenzo ya kuboresha maendeleo ya taaluma katika shule zao.
Hata hivyo, Mwalimu Bunonus amesisitiza umuhimu wa kila shule kuwa na vifaa vitakavyowezesha matumizi bora ya mfumo huo, ikiwemo Vishikwambi na Kompyuta, akibainisha kuwa shule ambazo hazina vifaa hivyo zitapatiwa.
“Suala la kuwa na vifaa vya kufanyia kazi ni la lazima. Ni aibu sana kumkuta Mwalimu Mkuu akifanya majumuisho ya taarifa za shule yake Stationary, wakati taarifa hizo zinapaswa kuwa siri. Kama kuna shule haina kompyuta, watanunuliwa,” amesema Bw. Bunonus.
Kwa upande wake, Afisa TEHAMA wa Wilaya ya Longido, Bi. Zaina Mzee, ametoa rai kwa walimu wakuu kuhakikisha wanawasilisha orodha ya vifaa walivyonavyo katika shule zao vinavyotumika kwenye mfumo huo, ili viwekwe katika kanzidata.
Naye Mwenyekiti wa Maafisa Elimu Kata wa Wilaya ya Longido, Mwalimu Dennis Byarugaba, ameshukuru kwa mafunzo hayo na kueleza kuwa katika wakati huu wa sayansi na teknolojia ni lazima kila mwalimu kuufahamu mfumo wa SIS.
Amebainisha kuwa wamepokea mafunzo hayo na watakwenda kuyatekeleza, huku akiwasihi walimu watakaokumbana na changamoto wakati wa kutumia mfumo huo wasisite kuuliza ili kuepuka vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatatekelezwa kwa weledi mkubwa katika shule zote wilayani humo.
@@
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: +255 272 970 793/ 94
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.