NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO
Jumla ya wanafunzi 219 wamehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Engarenaibor iliyopo Kata ya Engarenaibor Wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Wahitimu hao ni sehemu ya waafunzi 327 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2022 ambapo imeelezwa kuwa baadhi yao hawakuhitimu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za ujauzito, utoro na kuhama shule.
Akizungumza katika mahafali ya 16 yaliyofanyika Oktoba 3, 2025 shuleni hapo, Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwanabonde Investment Antony Mngodo alitoa wito kwa wanafunzi hao kufuta daraja la sifuri (Division 0) na kuhakikisha wanapata daraja la kwanza (Division I) na daraja la pili (Division II) katika mtihani wao wa NECTA unaotarajia kuanza Oktoba 13 mwaka huu.
Mngodo aliupongeza uongozi na waalimu wa shule hiyo kwa kuwaandaa vyema wanafunzi hao ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mtihani wao.
"Nawapongeza wanafunzi mliofikia hatua hii leo na Mungu awatunze hadi kwenye mtihani wenu. Nyie mmechaguliwa kufanya mtihani, hivyo mhakikishe mnafanya vizuri," alisema Mngodo na kuongeza,
"Walimu nawapongeza pia kwa kazi nzuri mliyoifanya na kuhakikisha mnafuta daraja sifuri kwa wanafunzi hawa, kufuta hizi sifuri ni mafanikio makubwa kwenu walimu. Tunawapongeza walimu kwa kazi hii kwani sio kazi nyepesi,".
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Longido Mwl. Gilbert Sombe alisema kuwa kutokana na maandalizi yaliyofanyika kwa wanafunzi hao kuelekea mtihani wao wa mwisho, hawategemei mwanafunza yeyote kupata daraja sifuri.
"Katika Shule hii tumepambana kuhakikisha tunaziondoa Division 0 (Daraja Sifuri), kwahiyo hatutegemei kuwa na sifuri," alisema Mwl. Sombe.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Honest Kilewo alisema kuwa idadi ya wanafunzi waliohitimu katika mahafali hayo ya 16 ni 219 na aliwahakikishia wazazi na wananchi kuwa kutokana na maandalizi makubwa waliyowafanyia watafanya vizuri mtihani.
Hata hivyo alitoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao hususan wanapokuwa nyumbani kipindi cha likizo kwani kuwa mbali nao kunachangia kuporomoka kwa maadili ya watoto ambapo ameeleza kuwa kwa kpindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu Shule hiyo imevunja rekodi ya kuwa na wanafunzi 17 waliopata ujauzito.
Kwamba wanafunzi waliopata ujauzito kwa kidato cha kwanza ni watatu (3), kidato cha pili watatu (3), kidato cha tatu 10 na kidato cha nne mmoja (1) na kufanya jumla kuwa wanafunzi 17.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.