Wilaya ya Longido imewataka wananchi wote ambao bado hawajajiandikisha kwenye orodha ya mpiga kura kutumia siku chache zilizobaki kuhakikisha wanajisajili. Lengo ni kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura anapata haki yake ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa 27 Novemba 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya, Bwana Jacob Lyimo alitoa wito huo alipokuwa akifuatilia maendeleo ya zoezi la uandikishaji katika kata za Olmolog na Tingatinga wilayani Longido. Alisisitiza kuwa vituo vya kujiandikisha viko wazi, na taratibu zote zimerahisishwa ili kuwawezesha wananchi wengi iwezekanavyo kufanikisha zoezi hilo.
Bwana Lyimo pia alifafanua kuwa zoezi hilo limeanza rasmi tarehe 11 Oktoba 2024 na litakamilika tarehe 20 Oktoba 2024. Vituo vya kujiandikisha vitakuwa wazi kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
"Ni muhimu kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura ajitokeze na kutumia nafasi hii ya mwisho ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi na michakato ya maamuzi ya maendeleo ya wilaya yetu na nchi kwa ujumla," alisema Lyimo.
Hii ni fursa muhimu kwa wananchi kushiriki katika kuamua mustakabali wa taifa, na hivyo kujiandikisha ni hatua ya msingi kuelekea kutimiza haki hiyo ya kikatiba.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM