Na. Zaina Mzee.
Mkuu wa wilaya ya Longido Mh Frank James Mwaisumbe leo tarehe 21/03/2019 katika ofisi ya kijiji cha Longido,amegawa vitambulisho vya matibabu kwa wazee wenye zaidi ya miaka sitini.Wazee zaidi ya themanini wamepata vitambulisho hivyo ikiwa ni kwa awamu ya kwanza tu.Mh Mwaisumbe amewaambia wazee hao kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha wanapata huduma za afya bure kwa kutambua mchango wao katika kujenge nchi enzi wakiwa vijana na sasa ni wakati wao kufurahia matunda ya nchi yao. aidha amewataka wazee hao kuhakikisha wanatunza vitambulisho vyao ili waweze kutibiwa na wasipate usumbufu wowote kwenye vituo vya afya. "wazee ni hazina na palipo na wazee hapaharibiki kitu natumai uwepo wenu kwenye nchi yetu ni baraka kubwa sana hata nasi vijana tunapo waona tunajivunia hivyo sisi kama serikali tunayo wajibu wa kuwatunza ninyi na mjione hii nchi inawatambua,hivyo basi nawasihi mpokee hivi vitambulisho mkavitunze viweze kuwasaidia katika matibabu yenu.Nataka kuwahakikishia serikali imejipanga kuhakikisha huduma za afya kwenu wazee ni bure,ukiugua chukua kitambulisho chako nenda ukatibiwe bure." alisema Mwaisumbe.
Nae afisa Ustawi jamii Wilaya ya Longido Bi. Atuganile chisunga ambaye ndiyo mratibu wa zoezi hilo alisema, "kwa kuanzia tumeanza na kata ya Longido na tunajipanga kuendelea na zoezi la kugawa vitambulisho vya Matibabu kwa Wazee wa wilaya nzima ya Longido kwa sababu tunawathamini sana wazee wetu kwani bila wao wazee sisi tusingekuwa hapa leo na hata nchi yetu isingefika hapa tulipo hivyo wazee ni hazina yetu kubwa sana na mna kila sababu ya kupata vitambulisho hivi na nitahakikisha wazee wote wa Wilaya hii ya Longido wanapata Vitambulisho vya kupatiwa matibabu bure".
Wazee hao nao wameshukuru kwa kupewa vitambulisho vya matibabu na kuishukuru serikali ya Rais John Pombe Magufuli kwa kutambua uwepo wao."Tunashukuru kwa serikali hii ya Mh Rais kwa kutambua uwepo wetu mimi kama mzee nimekuwa nikisumbuka hata kama nikipata homa inagharimu kuanza kutafuta hela ya kununua dawa lakini kwa kupewa kitambulisho hiki nina hakika tatizo langu litamalizika kabisa nishukuru sana serikali namshukuru Rais wetu mtetezi wa wanyonge anatupenda sisi wazee na mshukuru mkuu wetu wa wilaya" alisema Bibi Maria ole Karooi mwenye umri wa miaka 90.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM