Na Happiness Nselu
Longido, Februari 24, 2025* – Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli, ametoa wito kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo kufuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ya kazi, akisisitiza kwamba ni jukumu lao kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa elimu wilayani Longido, DC Kalli alisema kuwa serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, na kwamba ni muhimu kwa walimu wakuu kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa ipasavyo.
“Pesa zimeletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na ni wajibu wenu, walimu wakuu, kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora. Hii ni fursa nzuri kwa jamii yetu na hatuwezi kuvuruga matumaini ya wananchi kwa kutochukua hatua za haraka,” alisema DC Kalli.
Mkuu wa Wilaya aliongeza kuwa, ingawa wengi wanaweza kutokuwa na taaluma ya uhandisi, bado wanaweza kuona matatizo na kushirikiana na wataalamu ili kuhakikisha miradi inakamilika kama ilivyokusudiwa. Aliwataka walimu wakuu kuwa sehemu ya mchakato wa ufuatiliaji wa miradi hiyo, kwani wana nafasi ya karibu na jamii na wana uwezo wa kuona changamoto zinazojitokeza.
“Miradi ni muhimu kwa maendeleo ya wilaya yetu, na hatuwezi kuruhusu kazi kukwama kwa sababu ya kutokuwa na uangalizi. Hata kama huna taaluma ya uhandisi, ukiwaona watu wanachonga au kufanya kazi isiyokamilika, tafadhali fuatilieni. Hii ni kwa manufaa ya wilaya yetu,” alisema.
Kalli alisisitiza kwamba ufanisi wa miradi ya maendeleo unategemea ushirikiano wa karibu kati ya walimu, viongozi wa serikali, na wananchi. Alihimiza kuwa walimu wakuu na viongozi wa shule wawe na uchunguzi wa mara kwa mara kuhusu miradi inayotekelezwa kwenye shule zao na kutoa ripoti kwa wakati ili kuchukua hatua haraka.
Kauli ya DC Kalli imepokelewa vizuri na walimu, ambao wameahidi kuongeza ushirikiano na viongozi wa serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea bila matatizo. Viongozi wa elimu wilayani Longido wanatarajia kwamba hatua hizi zitachangia kufanikisha miradi bora, na hivyo kuleta maendeleo ya kudumu kwa jamii nzima ya Longido.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM