Na Hapiness Nselu
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro Shemzigwa, amefungua mafunzo ya siku moja kwa ajili ya waandishi wasaidizi na waendeshaji wa mashine za BVR, yatakayofanyika katika kata zote 18 za wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Julius Kambarage Nyerere uliopo makao makuu ya halmashauri hiyo, Bw. Shemzigwa aliwapongeza washiriki kwa kuaminiwa na kuteuliwa tena kushiriki katika utekelezaji wa jukumu hilo muhimu la kitaifa.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Mpiga Kura linatarajiwa kuanza rasmi Mei 16 hadi 22, 2025, katika kata zote 18 za Wilaya ya Longido.
“Mnatakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu, kutunza vifaa mlivyopewa, kuepuka vitendo vya uzembe au visivyofaa vinavyoweza kuhatarisha mchakato huu muhimu. Fanyeni kazi kwa weredi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,” alisisitiza Mkurugenzi.
Amesema lengo ni kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa anapata haki yake ya msingi ya kupiga kura na kuchagua viongozi anaowataka katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Serikali Kuu.
Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Longido, Bw. Nevviling Lymo, alisema ofisi yake itahakikisha inasimamia kwa karibu utekelezaji wa zoezi hilo ili lifanikishwe kwa viwango vya juu na kwa wakati uliopangwa.
“Ni wajibu wa kila afisa mwandikishaji kuhakikisha taarifa zote muhimu zinawasilishwa kwa wakati na mahali sahihi, na kushirikiana kikamilifu na watendaji walioko vituoni ili kufanikisha kazi hii,” alisema Bw. Lymo.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, *Mwenyekiti wa Mafunzo, Bw. Ernest Lotakajack , alisema wako tayari kuhakikisha zoezi linafanyika kwa ufanisi mkubwa na kuleta matokeo chanya katika jimbo hilo.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM