Na Happiness Nselu
*Longido, Machi 21, 2025* - Wataalamu kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe, wakiongozwa na Mratibu wa Elimu ngazi ya Jamii, Bw. Wasele, leo wamefanya ziara katika shule ya Sekondari Ketumbeine na Engarenaibor, kutoa elimu muhimu kuhusu ugonjwa wa mpox na magonjwa mengine yanayoathiri jamii.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Longido, Dkt. Dioniz Methew Majani, alisema kuwa idara yake imejipanga kikamilifu kukabiliana na ugonjwa wa mpox. Alisema kuwa kupitia utoaji wa elimu na mikutano ya jamii, wameweza kuhamasisha wananchi kuhusu hatua za tahadhari na jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi.
“Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe imejizatiti kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huu. Tunasisitiza umakini na ushirikiano kutoka kwa kila mmoja wetu katika kudhibiti mambukizi. Huduma za afya zipo, na tunahakikisha kwamba jamii inapata elimu ya kutosha kuhusu magonjwa haya,” alisema Dkt. Majani.
Bw. Wasele aliongeza kuwa, mbali na elimu kuhusu mpox, wamejizatiti pia kutoa huduma za lishe kwa wananchi. Lishe bora, alisema, ni muhimu katika kujenga kinga ya mwili dhidi ya magonjwa. Aidha, alisisitiza kuwa elimu hii ni sehemu ya juhudi kubwa za serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na lishe. Alisema kuwa, "Kwa kushirikiana, tunaweza kupunguza madhara ya magonjwa haya na kuhakikisha afya ya jamii inaboreshwa."
Ziara hii inatolewa kama sehemu ya mkakati wa serikali kuongeza ufahamu kuhusu magonjwa yanayoathiri jamii na kupunguza madhara yake kwa kupitia elimu, ushirikiano na huduma za afya bora. Idara ya Afya pia inaendelea kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na jamii kwa ujumla, ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi wote.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM