FURSA ZA KILIMO WILAYANI LONGIDO
Wilaya ya Longido, licha ya kuwa katika eneo la ukame na nusu-jangwa, ina fursa mbalimbali za kilimo ambazo zinaweza kutumika kikamilifu kwa maendeleo ya kiuchumi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Fursa hizo ni pamoja na:
1. Kilimo cha Umwagiliaji
Longido ina mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji maeneo ya Ngereyani na Tingatinga na kilimo cha mboga mboga, matunda na mazao ya biashara.
2. Kilimo cha Mazao ya Chakula
Mazao kama mahindi, maharage, Alizeti, na viazi Mviringo yanaweza kustawi katika maeneo yanayopata mvua ya wastani. Pia kuna fursa ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbegu bora na teknolojia za kisasa kama matrekta, pembejeo na huduma za ugani.
3. Kilimo cha Mazao ya Biashara
Wilaya inafaa kwa kilimo cha mazao ya biashara kama Ngano,Viazi mviringo, njegere na alizeti, hasa katika maeneo ya Eworendeke, Olmolog, Kamwanga,Tingatinga na Kimokouwa. Haya yanaweza kuongezwa thamani kwa usindikaji wa ndani na kuuza nje ya wilaya.
4. Kilimo cha Mboga na Matunda
Katika maeneo ya umwagiliaji, kilimo cha mboga kama nyanya, vitunguu, pilipili hoho, kabichi na matunda kinafanyika kwa mafanikio. Soko lake ni kubwa ndani na nje ya wilaya, hasa maeneo ya Arusha Mjini na Namanga.
5. Kilimo Hai na Kilimo Endelevu
Kutokana na mwamko wa wananchi wa kutunza mazingira, kuna fursa kubwa ya kuendeleza kilimo hai (organic farming) kinachotumia mbolea za asili, ambacho kinaweza kupata masoko ya kimataifa na kukuza kipato cha mkulima.
6. Uwekezaji kwenye Teknolojia ya Kilimo
Kuna fursa ya kuanzisha mashamba ya mfano, matumizi ya teknolojia za kisasa kama greenhouses, drip irrigation, matumizi ya drones kwa uchunguzi wa mashamba, na huduma za ugani za kidigitali kwa wakulima.
7. Uwezeshaji kwa Vijana na Wanawake
Programu nyingi za uwezeshaji kama 10% ya mapato ya Halmashauri, mkopo wa vijana na wanawake zinaweza kutumika kuanzisha vikundi vya kilimo vya kisasa, bustani za mfano, au miradi ya pamoja ya kilimo biashara.
8. Masoko ya Ndani na Nje
Kutokana na jiografia ya Longido kuwa mpakani na Kenya kupitia Namanga, kuna fursa ya kuuza mazao ya kilimo kwenye masoko ya kimataifa hasa Kenya. Pia barabara za kuunganisha wilaya na mikoa mingine zinaimarisha usafirishaji wa bidhaa za kilimo.
9. Uanzishwaji wa Vituo vya Ushauri na Mafunzo ya Kilimo
Wilaya inaweza kuanzisha vituo vya mafunzo ya kilimo kwa wakulima ili kuongeza tija. Ushirikiano na taasisi za kilimo kama SUA, TARI na NGOs unaweza kufanikisha hili.
Ukichanganya fursa hizi na mazingira ya kisiasa yaliyopo, usalama wa chakula na sera za kitaifa zinazounga mkono sekta ya kilimo, Wilaya ya Longido ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha kilimo endelevu cha kibiashara.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.