Na Happiness Nselu
Kamati za MTAKUWWA (Mpango wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto) katika ngazi ya kata zimeimarishwa kupitia mafunzo maalum yaliyofanyika Namanga, yakilenga kuongeza uelewa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Mafunzo hayo yalikutanisha wajumbe wa kamati, viongozi wa dini, viongozi wa kijamii pamoja na wadau wa maendeleo, ambapo washiriki walipata ujuzi kuhusu mbinu za kuzuia na kushughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia, huku wakisisitizwa kushirikiana kwa karibu na vyombo husika.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani Longido, Bi. Monica R. Wambura, alisema kuimarishwa kwa kamati za MTAKUWWA ni hatua muhimu ya kuhakikisha jamii inalindwa na vitendo vya ukatili.
“Kamati hizi ndizo silaha muhimu katika mapambano ya ukatili wa kijinsia. Kupitia mafunzo haya, zinapata uelewa wa sheria, haki za binadamu na mbinu za kuchukua hatua stahiki kwa haraka,” alisema Bi. Wambura.
Miongoni mwa mada zilizotolewa ni pamoja na chanzo cha ukatili wa kijinsia, wajibu wa jamii katika kulinda haki za wanawake na watoto, mbinu za kuripoti na kufuatilia matukio ya ukatili, pamoja na mikakati ya kijamii ya kuzuia vitendo hivyo.
Washiriki walieleza kuwa elimu hiyo imewaongezea ujasiri na maarifa ya kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha matukio ya ukatili yanatolewa taarifa mapema na hatua madhubuti kuchukuliwa.
Mafunzo haya yamewezeshwa na WASHEWILO kwa kushirikiana na Legal Services Facility (LSF) na Enabel, yakilenga kuimarisha jitihada za kijamii na kitaasisi katika kulinda haki na hadhi ya makundi yaliyo hatarini.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.