OPARESHENI YA JENGA CHOO TUMIA CHOO.
Mkuu wa Wilaya ya Longido , Mhe. Frank James Mwaisumbe ametoa agizo kwa maafisa Tarafa na watendaji wa vijiji vyote wilayani Longido kuwa anatoa miezi mitatu(3) tu,wahakikishe kila kaya (boma) ina choo, pamoja na sehemu zenye mikusanyiko ya watu kama vile sokoni, shuleni (msingi na sekondari).
Mh. mwaisumbe ameyasema hayo leo hii tarehe 22.08.2019 akiwa katika kikao cha afya na lishe kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Wilaya,Mh mwaisumbe ameongeza kuwa mtu yeyote atakaye kiuka agizo hili, kwa maana kuwa asijenge choo na kutumia choo atachukuliwa hatua za kisheria.
Pia Mh. Mkuu wa wilaya amewaagiza maafisa elimu (msingi na sekondari) kuwasimamia walimu wakuu wa shule na kuwahimiza mazingira kuwa safi na kuhakikisha kuwa wanatumia vyoo vizuri ili kuepuka uchafuzi wa mazingira na kuondokana na magojwa ya kuhara kama vile kipindupindu ndani ya wilaya yetu ya Longido. Amesema kuwa kufikia mwakani Longido haitakiwi kuwa katika namba ya 166 ndani ya wilaya 184 Tanzania kwani kila kitu kinawezekana tukiamua, Mh. Mwaisumbe amewataka maafisa tarafa kutoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa vyoo na matumizi yake kila baada ya mwezi mmoja. Pia amewaasa maafisa tarafa kushirikiana na idara ya afya pamoja na maendeleo ya jamii kuwa na ratiba ya kuelimisha jamii juu ya afya na umuhimu wa vyoo katika jamii.
Nae afisa afya mkoa wa Arusha Vones z Uiso ameeleza jinsi gani operesheni hii ya vyoo ilivyo weza kubadilika toka kuanzishwa mwaka 2012 hadi 2015. Amesema kuwa operesheni hii ya awamu ya pili mwaka 2017 hadi 2019 imekuwa na maendeleo mazuri mkoani Arusha hadi kufikia 81% kwa kuwa na vyoo. Katika kuelezea changamoto ya afya amesema kuwa mila na desturi potofu zimechangia jamii kutokuwa na vyoo, pia ameeleza uhaba wa maafisa wa afya katika ngazi ya mkoa kwani wana uhitaji wa watu 155 huku maafisa afya jumla wako 102 hivyo kuna changamoto katika kutaka kuwafikia watu wote katika kila kijiji na ndio maana wanaomba kusaidiana na watu wote ili kuwa na afya bora.
Pia Afisa lishe wilaya Adelin kahija ameeleza baadhi ya changamoto katika ngazi ya wilaya kama ukosefu wa vitendea kazi kwa wataalamu wa lishe, ukosefu wa rasilimali fedha. Amesema kuwa anaunga mkono agizo la Mkuu wa wilaya kuhakikisha kila kaya ina kuwa na choo.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM