Leo tarehe 01-10-2019 katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya Longido imefanyika sherehe ya kuhitimisha kilele cha siku ya wazee ambayo kimkoa imefanyika hapa wilayani Longido na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Ndugu Toba Nguvila ambaye ni katibu tawala wa wilaya pamoja na wazee wote kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Arusha. Kwenye maadhimisho hayo wazee walipata nafasi ya kusoma risala fupi mbele ya mgeni rasmi ndugu Toba nguvila ambayo ilielezea hali ya wazee kimkoa na kiwilaya, mambo ambayo wanatekeleza kama baraza, mikakati na changamoto mbalimbali wanazozikabili kama ifuatavyo;-
Mheshimiwa Mgeni rasmi.
Awali ya yote nipende kumshukuru Mungu kwa kukuwezesha kuungana nasi kwenye tukio hili muhimu kwa wazee wetu, Hakika umeacha majukumu mengine na kulipa jukumu hili kipaumbele.
Huduma za ustawi wa jamii zimekuwa zikiratibu pamoja na mambo mengine masuala ya wazee , kwa kuzingatia sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003, Sera ya Afya 2007 na Miongozo mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha wazee wanastawi vyema na kupatiwa fursa sawa pasipo kubaguliwa kwa namna yeyote ile.
Maadhimisho ya mwaka 2019 Kitaifa yanafanyika Mkoani Mtwara na yamebeba kauli mbiu isemayo “TUIMARISHE USAWA KUELEKEA MAISHA YA UZEENI”. Ujumbe huu una maana kubwa sana hasa ukizingatia kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili unaopelekea wazee wetu kukosa uangalizi na kuwa kundi lililotengwa, kama kutakuwa na usawa na malezi bora kwa wazee hatutegemei kuwa na makao ya wazee kwani wazee ni vizuri wakalelewa katika ngazi ya familia, kwani uzee na kuzeeka hakuna wa kuukwepa.
MAMBO YALIYOTEKELEZWA
Tumeendelea Kuhamasisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa Wazee kwa kuweka matangazo katika hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati yanatoa ujumbe usemo ‘MZEE KWANZA: MPISHE MZEE APATE HUDUMA’ ikiwa ni njia ya kutoa huduma kwa haraka kwa Mzee katika vituo vyetu vyote vya huduma.
Jumla ya mabaraza 548 kati ya 687 yameundwa katika ngazi mbali mbali ndani ya Mkoa wa Arusha kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi ngazi za Mkoa sawa na asilimia 80%.
Mkoa umeitikia agizo la kuwatambua wazee kama ilivyo kwa makundi mengine muhimu nchini mwetu na Hadi sasa jumla ya wazee 64,999 wametambuliwa ,
Mkoa umefikia 52% ya utoaji wa vitambulisho kwa wazee na tumeazimia ifikapo mwezi March 2020 kila Halmashauri iwe imekamilisha zoezi hili kwani fedha zimetengwa kwenye mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Jumla ya wazee 8 na maafisa ustawi 4 wameweza kushiriki katika maadhimisho ya wazee Kitaifa Huko Mkoani Mtwara ambapo Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mgeni rasmi.
Mkoa umeweza kuwapatia wazee Ofisi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za Baraza.
BARAZA LA WAZEE MKOA
Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 inasisitiza kwamba “YATAUNDWA MABARAZA YA USHAURI WA WAZEE KATIKA NGAZI ZA VIJIJI/MITAA, KATA, WILAYA, MKOA NA TAIFA”
Mnamo tarehe 08/12/2018 Mkoa uliendesha kikao maalum cha uchaguzi wa baraza la wazee ambapo jumla ya Halmashauri tano (5) kati ya saba (7) zilishiriki na kuchagua uongozi wake
Baraza la wazee mkoa wa Arusha linaundwa na jumla ya wazee 49 yaani wazee saba kutoka kila Halmashauri, na linaviongozi saba wakiwemo mwenyekiti, makam, katibu, makamu, mhazini, na wazee wawili Me na Ke.
MAJUKUMU YA BARAZA
Mwongozo na majukumu ya mabaraza ya wazee ngazi ya vijiji/mtaa, kata, wilaya, mkoa na taifa unafafanua juu ya hili kupitia matamko na vifungu mbalimbali kwenye sera ya wazee kama inavyoonekana
Ibara ya 3.14-.3.15 na, Sura ya 4, Ibara ya 4.1 – 4.4)
Kufanya Mkutano wa Baraza la Wazee la Mkoa kila baada ya miezi 6. Kwa maana hiyo Baraza la Mkoa litakutana Mara mbili (2) kwa Mwaka.
Kusimamia utoaji wa huduma kwa Wazee katika halmashauri zote.
Kuhimiza Halmashauri, Asasi na Wakala za Hiari ili kutoa huduma mbalimbali za msingi kwa Wazee wote wa miaka 60 na kuendelea.
Kushauri Serikali kuwa na mwakilishi wa Wazee kwenye Bunge kama ilivyo kwa makundi ya wanawake, Walemavu na vijana.
Kupokea kero mbalimbali za Wazee kutoka kwenye halmashauri zote na kuzitafutia ufumbuzi.
Kuchagua wawakilishi wawili watakaoshiriki katika kuunda Baraza Huru la Wazee la Taifa.
Kuratibu shughuli za Mabaraza ya Wazee ya kila halmashauri na lile la Mkoa
Kushiriki na kutoa mawazo kwenye vikao, mikutano na hafla mbalimbali ngazi ya mkoa.
Mabaraza yatadumu kwa muda wa miaka 3
CHANGAMOTO
Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mkoa na Serikali ya Tanzani kwa ujumla kwa kushirikiana na wadau katika kutoa huduma stahiki kwa Wazee, bado eneo hili linakabiliwa na changamoto ambazo zinahitaji kushughulikiwa kwa pamoja:
Uchache wa Maafisa Ustawi wa Jamii kwenye ngazi ya Halmashauri hasa kwenye kata na vijiji ambako hakuna Afisa Ustawi wa jamii hata mmoja, Wilaya ya Longido ina afisa ustawi wa jamii mmoja tu ambapo leo tunaadhimisha siku hii muhimu.
Baadhi ya Halmashauri Kutokutenga vyumba na madaktari mahsusi wa kutoa huduma za Afya kwa wazee kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati
Upatikanaji duni wa madawa kwa ajili ya magonjwa ya Wazee na huduma za Mkoba kwa Wazee
Uchache wa wadau katika eneo la Wazee na Walemavu.
Ufinyu wa bajeti za masuala ya wazee na huduma za Ustawi wa Jamii ngazi za Halmashauri
Kutokamilika vitambulisho vya wazee kwa baadhi ya halmashauri kama jedwali lilivyoonyesha hapo juu kwani ni 52% tu ndio wenye vitambulisho.
3: MIKAKATI
Kuhakikisha mabaraza ya wazee Mkoa na Wilaya yanapatiwa mafunzo juu ya majukumu yao, kwa sasa tupo kwenye mazungumzo na wenzetu wa Helpage kuona namna ya kuratibu na kuwezesha mafunzo haya.
Uongozi wa wazee kushawishi masuala ya wazee kujadiliwa katika vikao muhimu kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Wilaya ili kuongeza msukumo wa utekelezaji wa mahitaji yao.
Kuhakikisha zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Wazee unakamilika katika Wilaya Zote hasa (Karatu na Longido) ambapo takwimu zinaonyesha wapo chini.
Kuwahimiza wazee kuunda vikundi vidogo vidogo vya kijasiriamali na kifugaji kwa ajili ya kuzalisha mali jambo ambalo litawasaidia kupata mahitaji yao madogo madogo ya kila siku.
HITIMISHO
Tunakushukuru wewe binafsi kwa kukubali kuungana nasi katika siku hii muhimu kwa wazee wetu, Nitoe shukrani pia kwa Viongozi wote wa Mkoa, wilaya na Halmashauri kwa ushirikiano waliouonyesha kufanikisha sikua hii, kipekee niwashurkuru viongozi wa baraza la wazee Mkoa ambao jitihada zao za kuona siku hii inafanyika hapa Wilayani Longido zimezaa matunda.
Mwisho Ndugu mgeni rasmi alimalizia kwa maneno machache akisema
Ninapenda kuwatakia kila la kheri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi November na ninaamini tutashiriki vyema na kutumia haki yetu ya Kikatiba vizuri, ninaahidi kushirikiana na Viongozi wote wa Baraza kwa Lengo la kuboresha huduma kwa wazee wetu ndani ya Mkoa wetu,
Nawashukuru wazee kwa kunipa jukumu la kulea baraza la wazee Mkoa baada ya kuniomba wakati wa uzinduzi ninawaahidi kazi, pia Ninawashukuru wote walioandaa maadhimisho haya, wakiwemo Viongozi wa wazee, Mganga Mkuu wa Mkoa na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya kwa kuwawezesha baadhi ya wajumbe mliopo hapa kufika, pia wataalam wa serikali hasa maafisa ustawi wa jamii kwa kushiriki kwenu kikamilifu mwenyezi mungu awabarika sana.
Tunazitambua juhudi hizi kama mchango katika kuwajali wazee na ninaomba ziendelezwe pia niwaombe kwa namna ya kipekee tuendelee kuliombea Taifa letu na viongozi wetu chini ya Mh Rais Dr John Pombe Magufuli ili kazi nzuri anayoifanya iendelee kuboreka na wananchi wetu waendelee kustawi vyema tunapoelekea kwenye uchumi wa kati.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM