Leo tarehe 27-11-2019 msimamizi mkuu wa uchaguzi wa serikali zavijiji na vitongoji Jimbo la Longido Bi Natang’aduak Zakayo Mollel amelisimamia zoezi nzima la kuwaapisha viongozi mbalimbali vijiji na vitongoji katika ukumbi wa JK Nyerere ulioko hapa Halmashauri ya Longido. Katika zoezi hilo Hakimu mkazi wa mahakama ya mwanzo wilaya Longido Ndugu Shila Mkoma Dyumu aliwaapisha takribani viongozi 1225 ikiwemo wenyeviti wa vijiji 49,wenyeviti wa vitongoji 176,wajumbe wa kundi mchanganyiko 608 na wajumbe wa viti maalum 392 kutoka katika vijiji na vitongoji mbalimbali wakiwa wanatoka Chama Cha Mapinduzi CCM.
Pia utoaji wa viapo ulishuhudiwa na katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya Ndugu Ezekiel Mollel, mwakilishi wa mkuu wa wilaya,afisa kupambana na kuzuia Rushwa Takukuru wilaya Ndugu Ally Mikidadi ,mwakilishi wa OCD,viongozi wa dini na wataalam wa idara na vitengo mbalimbali vya Halmashauri.
Bi.Natang’aduaki Mollel alitumia nafasi hii kuwapongeza sana viongozi hao kwa kupata kibali cha kupewa nafasi ya kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka minne na kuwataka waende wakatatue kero mbalimbali za wananchi na kufanya kazi kwa uadilifu na utii bila upendeleo wowote. Pia alitoa shukrani kubwa sana kwa ushirikiano alioupata kutoka kwa watendaji mbalimbali kabla na wakati wa uchaguzi kwani zoezi la uchaguzi lilienda vizuri hakukua na vitendo vyovyote vya kuonewa, kupendelewa na uvunjivu wa amani.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya Longido Ndugu Ezekiel Mollel pia aliwapongeza viongozi hao wateule kwa kupata dhamana ya kuwaongoza wananchi na kuwataka waende kuwatumikia wananchi na kutatua kero ambazo zinawafanya wananchi kuichukia na kutoipenda CCM ili kukifanya chama kiweze kukubalika na kupata dhamana tena kwenye chaguzi zijazo. Pia aliwataka kuacha kukisema vibaya chama kwani ndicho kilichowaweka madarakani na kuacha vitendo vya rushwa kwenye kuwatumikia wananchi na kutosita kuwaondoa na kuwafukuza viongozi wazembe kwenye chama.
Mwakilishi wa OCD wilaya pia aliwapongeza viongozi wateule kwa kupata nafasi ya kuwatumikia wananchi na kusema kuwa kutokana na katiba yetu mimi sina chama kazi yangu kubwa ni kuhakikisha wananchi wanafuata sheria bila kulazimishwa endapo itaoneka unavunja sheria basi tunakukamata. Pia aliwataka viongozi waende kusimamia ulinzi na usalama kwenye maeneo yao kwa kuanzia kamati ya ulinzi na usalama katika maeneo wanayoyaongoza na kukemea vitendo viovu ikiwemo rushwa, ndoa za utotoni na wahamiaji haramu.
Afisa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa Ndugu Ally Mikidadi aliwapongeza viongozi wateule na kuwaambia kuwa leo mmekuja kula kiapo maana yake ni kwamba unaingia mkataba na serikali hivyo basi ukikutwa na kosa lolote lile uko tayari kushtakiwa kulingana na sheria na taratibu za nchi. Pia aliwataka viongozi wakawe mabarozi wazuri wakukemea na kutokomeza rushwa katika maeneo yao ikiwemo kwenye maswala ya ardhi na kwenye kuwatumikia wananchi kwani rushwa inasababisha vifo na upendeleo kwenye jamii.
Mwisho Bi Natang’aduak alimalizia kwa kuwasihi wenyeviti na wajumbe mbalimbali wakafanye kazi kwa ushirikiano na kuwa mstari wa mbele katika kuwatatulia wananchi kero zao na kuwafichua wale wote wanaofanya vitendo viovu ikiwepo kuwaficha Watoto wanaotakiwa kuanza shule, ndoa za utotoni na ukeketaji.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM