Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Salumu Kalli, ametoa wito kwa watumishi wa huduma za afya kote nchini kutumia lugha nzuri na yenye staha wanapohudumia wateja wanaofika kwenye vituo vya afya. Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi cha Mkoa kilichojadili vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga, kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere Wilayani Longido, Mheshimiwa Kalli alisisitiza umuhimu wa mawasiliano mazuri kati ya watoa huduma na wagonjwa.
“Lugha nzuri ni sehemu muhimu ya huduma bora kwa wateja. Inasaidia kujenga imani, kupunguza hofu, na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa. Nawataka watumishi wote wa sekta ya afya kote nchini kuelewa kwamba wagonjwa wanapofika katika vituo vya afya, wanahitaji si tu matibabu bali pia faraja na heshima,” alisema Mheshimiwa Kalli.
Kikao hicho kilikusanya wataalamu wa afya, viongozi wa serikali, na wadau mbalimbali ili kutathmini changamoto na suluhisho za kudhibiti vifo vya mama na mtoto. Mheshimiwa Kalli aliwataka washiriki kuhakikisha kwamba mbinu za kuboresha huduma zinatiliwa mkazo, ikiwa ni pamoja na kuboresha mawasiliano na wagonjwa.
“Ni jukumu letu wote kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa kwa kila njia, na hilo linaanza na jinsi tunavyowasiliana na kuwahudumia wateja wetu,” aliongeza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Simon Oitesoi, amewataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo yatakayotolewa na wawezeshaji ili kuleta matokeo chanya katika huduma ya afya.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro Shemzigwa, amepongeza juhudi za Idara ya Afya kwa kuchagua Longido kama mwenyeji wa mafunzo hayo muhimu. Bw. Shemzigwa alieleza kwa furaha kuwa, “Ni heshima kubwa kwa Wilaya yetu kuwa mwenyeji wa mafunzo haya. Nawakaribisha kwa mikono miwili na nina matumaini kuwa maarifa mtakayoyapata yatachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wetu.”
Kikao hiki kinatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga katika Mkoa wa Longido na maeneo mengine nchini.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM