Na Happiness Nselu
Leo, Tarehe 7 Novemba 2024, katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Halmashauri ya Wilaya ya Longido imefanya kikao cha mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa E-Board kwa watumishi wa halmashauri pamoja na Baraza la Madiwani la Wilaya ya Longido. Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Katibu Tawala wa Wilaya, Bi. Rahma Kondo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bi. Rahma Kondo alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi na madiwani wa wilaya, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia katika shughuli za uongozi na utawala ni muhimu kwa kuongeza ufanisi, kuboresha uwazi, na kupunguza ucheleweshaji katika maamuzi. Aliongeza kuwa mfumo wa E-Board utasaidia kuharakisha mchakato wa usimamizi wa mikutano na kutoa taarifa kwa wakati unaotakiwa.
Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo watumishi na madiwani katika matumizi ya mfumo wa kisasa wa kidijitali katika vikao vya Halmashauri na Baraza la Madiwani, ili kuwezesha ushirikiano bora na utoaji wa huduma za utawala kwa ufanisi zaidi.
Nae Mhe.Simon Oitesoi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido ameupongeza uongozi wa Halmshauri kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo muhimu kwa Madiwani na kuahidi kusimamia vema utekelezaji wa mfumo huo na kuongeza ufanisi katika mikutano.
Viongozi na washiriki wa mafunzo wamesema kuwa hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha utendaji kazi wa halmashauri unakuwa bora na unalingana na maendeleo ya teknolojia duniani.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM