NA ABRAHAM NTAMBARA, LONGIDO
Jumla ya wanafunzi 5,188 wa Darasa la Nne wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa Kitaifa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, mkoani Arusha kuanzia kesho Oktoba 22 hadi 23, 2025.
Akizungumza leo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Bw. Peter Matemba, amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika huku wanafunzi wakiwa tayari kwa mtihani huo muhimu katika safari yao ya kielimu.
“Kama wilaya tumejipanga vizuri, wanafunzi wameandaliwa vya kutosha. Tunawaomba wazazi wawaandae watoto wao vizuri na kuhakikisha wanafika shuleni mapema kwa ajili ya kufanya mtihani. Vilevile, tunatoa wito kwa wanafunzi wenyewe kujiandaa kwa bidii,” alisema Bw. Matemba.
Kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 2,726 na wasichana 2,462. Mtihani huo utafanyika katika shule 70, zikiwemo shule 57 za serikali na 13 zinazomilikiwa na mashirika ya dini pamoja na shule binafsi.
Bw. Matemba aliongeza kuwa walimu wakuu wameelekezwa kuandaa mazingira rafiki kwa ajili ya mtihani huo na kwamba semina mbalimbali zimefanyika kwa ajili ya kuwaandaa wasimamizi wa mitihani kuhakikisha uendeshaji wake unafanyika kwa ufanisi.
"Maandalizi yote muhimu tumeyakamilisha. Tunawatakia heri na baraka wanafunzi wetu wote katika upimaji huu wa kitaifa," aliongeza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Longido, Mwalimu Donat Bunonus, alisema wanafunzi wamepewa maandalizi ya kutosha na ana imani kuwa watafanya vizuri.
“Naomba wazazi wawaruhusu watoto wao kufika shuleni kwa wakati, na kwa wanafunzi nawahimiza wajibu mitihani yao kwa kuzingatia yale waliyojifunza kutoka kwa walimu wao,” alisema Mwalimu Bunonus.
Mtihani huu wa Upimaji wa Kitaifa ni kipimo muhimu cha kutathmini uwezo wa wanafunzi na kuandaa msingi bora kwa maendeleo yao ya kitaaluma.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.