Na Happiness Nselu
Kikao kazi cha tathmini ya lishe kilichofanyika leo katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Longido, kikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Salum Kalli.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Kalli alisisitiza umuhimu wa lishe bora kwa jamii, akieleza kwamba afya ya mama na mtoto inategemea sana mlo kamili na usawa. Alisisitiza pia kuwa, ni muhimu kwa kina baba kushiriki kikamilifu katika kujenga afya ya familia zao, hususan katika kuhakikisha mlo bora kwa wake zao na watoto wao.
Afisa Lishe wa Wilaya Bi. Adelina Kahija alisoma tathmini ya lishe katika wilaya, akionyesha mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuboresha lishe kwa jamii. Aliwahimiza viongozi na wananchi kuongeza jitihada za kutoa elimu zaidi kuhusu mlo bora, ili kupambana na utapiamlo na magonjwa yanayotokana na lishe duni.
Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Deoniz Mathew Majani, alitoa shukrani kwa wajumbe wa kikao hicho kwa kazi yao ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa mlo kamili.
Alisisitiza kuwa jamii inahitaji kuendelea kuwa na uelewa wa juu kuhusu lishe bora na akasema kwamba ni muda sasa wa kuhamasisha jamii kuhusu hatari ya wamama kujifungulia nyumbani, na umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya afya kwa usalama wa mama na mtoto.
Aidha, Dkt. Deoniz Mathew Majani alizungumza kuhusu huduma ya "M-Mama" inayotolewa na Serikali ambayo ni huduma ya usafirishaji wa wamama wajawazito na watoto wenye mahitaji maalum kutoka vijijini hadi vituo vya afya.
Alisisitiza kuwa huduma hii ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto, na alitoa wito kwa watendaji wa kaya na vijiji kuwa na madereva jamii watakaorahisisha upatikanaji wa huduma hii kwa haraka na ufanisi. Alisema kuwa ni muhimu kuhakikisha kwamba huduma za usafiri zipo karibu na wananchi, ili kuepusha vifo vya uzazi na madhara yanayoweza kutokea kutokana na ucheleweshaji wa huduma za afya.
Kikao hicho kilihudhuriwa na watumishi wa Halmashauri pamoja na watendaji wa serikali, na kililenga kuimarisha ushirikiano wa pamoja katika kuhakikisha wilaya ya Longido inakuwa na lishe bora na huduma bora za afya kwa wote.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM