Na Mwandishi Wetu, LONGIDO
VIONGOZI wa dini wilayani Longido wamewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na kupuuza taarifa za uvumi kuhusu maandamano, wakisisitiza umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Tamko hilo limetolewa leo na Kamati ya Haki na Amani ya Wilaya ya Longido katika kikao kifupi cha majadiliano kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya, kikihusisha viongozi wa dini zote kwa lengo la kuhimiza mshikamano na utulivu kuelekea uchaguzi huo.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini, Sheikh wa Wilaya ya Longido, Sheikh Ramadhani Mpangala, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema wananchi wanapaswa kuepuka kushiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake kutumia fursa ya uchaguzi kuchagua viongozi wanaowataka kwa uhuru na utulivu.

“Tunaomba waumini na wananchi wote muendelee kudumisha amani. Msisikilize taarifa za uvumi kuhusu maandamano. Badala yake, mjitokeze kwa wingi siku ya Oktoba 29 kupiga kura kuchagua viongozi mnaowataka,” alisema Sheikh Mpangala.
Aidha, aliwaonya wananchi watakaojaribu kushiriki katika vitendo vya vurugu au uchochezi kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria na mamlaka husika, akisisitiza kuwa amani ya nchi ni jambo lisilopaswa kuchezewa.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Haki na Amani, ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Simon Ole Morris, alisema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote, hivyo maandamano yasiyo na tija yanaweza kuvuruga utulivu na ustawi wa jamii.
“Watu wanaopanga kufanya maandamano wana nia ya kurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu. Hakuna sababu yoyote ya kuandamana. Badala yake, watu wote waandamane kwenda kupiga kura,” alisema Mchungaji Morris.
Naye Katekista Aidan Couman kutoka Kanisa Katoliki, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, alisema kwa mujibu wa maandiko matakatifu, Mungu anawaagiza waumini wote kuishi kwa amani na watu wote, hivyo kushiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.
Viongozi wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mchungaji Elikana Paresso wa Kanisa la Anglikana na Mchungaji wa Kanisa Halisi la Mungu Baba Amani Halisi, ambao kwa pamoja waliwasisitizia wananchi, viongozi wa dini na serikali kushirikiana kulinda amani na utulivu wa taifa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Mchungaji Amani Halisi alihitimisha kwa kuwataka wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura kutumia haki yao ya kikatiba Oktoba 29, 2025, kuchagua viongozi watakaoliwakilisha kwa kipindi kijacho cha miaka mitano, akisema “kura ni silaha ya amani.

Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.