Saratani ya mlango wa kizazi ni ugonjwa ambao umekuwa ukisababisha mateso na vifo vingi kwa wanawake.
Hayo yamesemwa leo tarehe 27/04/2018 na Mkuu wa wilaya ya Longido Mh. Daniel G. Chongolo wakati wa uzinduzi wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 14 na maadhimisho ya wiki ya chanjo kiwilaya yaliyofanyika Katika kituo cha Afya Longido.
Mh. Chongolo amewaasa wasichana kuacha kujamiiana katika umri mdogo kwani hiyo imekuwa ni moja ya sababu inayochangia saratani ya mlango wa kizazi.
Aidha Mh. Chongolo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wasichana wote waliofikia umri wa miaka 14 wanapatiwa chanjo hiyo ili kuwaepusha na hatari ya kuja kuathiriwa na ugonjwa huo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Afisa Elimu Wilaya Ndg. Gerson Mtera amewataka wasichana hao kuwa wajasiri ili waweze kupata chanjo hiyo na kuwakinga na madhara makubwa yanayoweza kuwapata.
Akitoa maelezo ya chanjo hiyo Mratibu wa huduma ya mama na mtoto Wilaya Ndg. Josiah Mruve amesema walengwa wa chanjo Kwa mwaka huu wa 2018 ni wasichana wote waliotimiza miaka 14, na kwamba kwa wilaya ya Longido matarajio ni kuchanja wasichana 2,271 kulingana na sensa iliyofanyika Katika shule zote na katika jamii.
Kwa upande wake mwanafunzi Sara Joel Laizer amabye amekuwa wa kwanza kupatiwa chanjo hiyo katika wilaya ya Longido ameishukuru serikali kwa kuwajali watoto wa kike na kuona umuhimu wa kutoa chanjo hiyo ili kuwakinga na athari ya saratani hiyo ya mlango wa kizazi.
Amesema wanawake wengi wanakufa Kwa ugonjwa huu wa Kansa ya mlango wa kizazi jambo ambalo lingeachwa liendelee lingekuwa na madhara makubwa kwa jamii.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM