Na Happiness Nselu
Shirika la Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TPW) limeanzisha mpango mkakati wa kutoa mafunzo kwa jamii katika vijiji vya Kimokouwa na Eworendeke wilayani Longido, kwa lengo la kuimarisha usalama wa binadamu na wanyama pori.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Meneja wa Shirika hilo, Bw. Envis Kisimiri, alieleza kuwa changamoto za mwingiliano kati ya binadamu na wanyama pori zimeendelea kuongezeka, hasa ikizingatiwa kuwa Longido ni mojawapo ya maeneo muhimu ya makazi na mapitio ya wanyama pori.
“Mafunzo haya yanalenga kuwasaidia wakazi wa maeneo haya kujua njia bora za kujikinga dhidi ya wanyama pori, huku tukihakikisha wanyama wanabaki salama. Tunataka kufanikisha ushirikiano wa kudumu kati ya binadamu na mazingira,” alisema Bw. Kisimiri.
Shirika la TPW limeeleza kuwa mpango huu ni sehemu ya jitihada za muda mrefu za kupunguza migogoro inayotokana na mwingiliano wa binadamu na wanyama pori, ambayo mara nyingi huleta madhara kwa pande zote. Mafunzo haya yanatarajiwa kuwahamasisha wanajamii kutumia mbinu salama kama vile ujenzi wa vizuizi imara, ufugaji wa mbwa wa kufukuza wanyama hatari, na matumizi ya teknolojia njia ya kitamaduni na kufuatilia mienendo ya wanyama pori.
Kwa niaba ya wakazi wa Kimokouwa na Eworendeke, Bw. Elianis Salaashe amepongeza juhudi za TPW, akibainisha kuwa elimu hiyo ni ya msingi kwa usalama wa maisha na mali zao. Alisisitiza kuwa mwingiliano na wanyama kama simba na tembo umekuwa changamoto kubwa, na kwamba mafunzo haya yamewapa maarifa ya kukabiliana na changamoto hizo kwa njia endelevu.
Bw. Salaashe aliongeza kuwa mafunzo haya pia yameimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi wanyama pori, si tu kwa usalama wao bali pia kwa faida ya kiikolojia na kiuchumi, ikiwemo utalii ambao ni chanzo muhimu cha mapato.
Mpango huu wa TPW unatazamiwa kupanuka hadi vijiji vingine wilayani Longido, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kufanikisha lengo la kuimarisha usalama wa binadamu na hifadhi endelevu ya wanyama pori. Pia, mipango ya ziada inajumuisha kuanzisha vikundi vya walinzi wa jamii kwa ajili ya kuimarisha usalama zaidi na kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wanajamii.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM