Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Salumu Kalli, leo tarehe 30 Septemba 2024, ameshiriki zoezi la ugawaji wa dawa za kingatiba dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, kama vile trakoma na vikope, katika kata ya Kimokouwa, wilayani Longido. Halmashauri ya Wilaya ya Longido, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali, imeendelea na mpango wa kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kama vile minyoo ya tumbo, kichocho, vikope, usubi, na mabusha.
Magonjwa haya yamekuwa yakiathiri jamii, hasa zile zenye kipato cha chini na zinazokaa kwenye maeneo yenye upatikanaji mgumu wa huduma za afya. Mradi wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele umegawanyika katika sehemu mbili. Kwanza, utoaji wa dawa za minyoo na kichocho kwa watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 14, na pili, utoaji wa dawa za vikope kwa watu wote isipokuwa watoto chini ya miezi sita, wajawazito, na wagonjwa mahututi.
Mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele wilayani Longido, Dk. Felix Mbise, akisoma taarifa ya umezeshwaji wa dawa za vikope, amesema kuwa mwaka 2022, zoezi la utoaji dawa kwa watoto lilifanikwa kwa asilimia 97.1, huku kwa watu wazima likifikia asilimia 88.6. Mwaka huu 2024, awamu ya kwanza imewafikia watoto 30,456 wenye umri wa miaka 5-14, huku watu wazima walengwa wakiwa ni 181,720. Awamu ya pili inatarajiwa kuwafikia walengwa 212,176, na zoezi la umezeshwaji wa dawa bado linaendelea kwenye kata zote wilayani Longido.
Akizungumza na wakazi wa kata ya Kimokouwa, Mheshimiwa Kalli amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kumeza dawa hizo za kingatiba kwa manufaa ya afya zao na jamii kwa ujumla. "Niwaombe ndugu zangu tujitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hili kwa ajili ya afya zetu. Bila kuwa na afya njema, huwezi kushiriki shughuli zozote za kimaendeleo, hivyo tuzilinde afya zetu," alisema Mheshimiwa Kalli.
Kwa upande wake, kiongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai, Laigwanani Ngulupa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia dawa za kingatiba dhidi ya trakoma na vikope, magonjwa ambayo yamekuwa yakiwasumbua wafugaji, hususan katika maeneo yao ambako magonjwa haya huenea kupitia wadudu kama inzi. "Ninamshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Longido kwa kuja kwenye boma letu na kugawa kingatiba dhidi ya trakoma. Nawaomba wananchi wenzangu kujitokeza na kumeza dawa hizi kwa afya zetu," alisema Mzee Ngulupa.
Umezeshwaji wa dawa za Trakoma na vikopr ni zoezi endelevu kwa wananchi na wakazi wa Longido.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM