Leo tarehe 27-02-2020 Naibu waziri wa Ujenzi uchukuzi na mawasiliano Mh Atashasta Justus Nditiye akiambatana na wataalamu kutoka TTCL na TCRA amefanya ziara wilayani Longido ya kufungua mnara wa mawasiliano uliopo katika kata ya Mundarara ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya TTCL ya kuwasha mawasiliano kwa wote Tanzania.
Katika ziara hiyo Mhe Atashasta Justus Nditiye alipata fursa ya kufanya kikao kifupi na uongozi mzima wa wilaya ya Longido uliochini ya Mkuu wa wilaya Ndugu Frank Mwaisumbe pamoja na Mbunge wa jimbo la Longido Dk Stephen Kiruswa na kupokea taarifa fupi ya hali ya miundombinu ya mawasiliano kwa ujumla katika ofisi ya mkuu wa wilaya kabla ya kwenda katika kata ya Mundarara kuzindua mnara wa mawasiliano.
Nae Dk Stephen Kiruswa mbunge wa jimbo la Longido na Mhe Elias Mushao Diwani wa kata ya mundarara walipata nafasi ya kumuomba mhe waziri wa ujenzi na uchukuzi juu ya ubovu wa barabara na sekta nzima ya mawasiliano katika baadhi ya vijiji na vitongoji.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika mawasiliano ndugu Waziri Kindamba kwa niaba ya timu nzima ya TTCL alimpongeza sana naibu waziri kwa kukubali wito wa kuambatana nao katika uzinduzi wa mnara wa mawasiliano ulio na kampeni ya washa mawasiliano kwa wote pia kuishukuru sana serikali kwa kusaidia katika kuimarisha huduma ya mawasiliano yenye tija Zaidi kwa wananchi.
Pia aliwataka wananchi kuhakikisha wanaiunga mkono serikali kwa kutumia mtandao wa TTCL kwani ni shirika la kizalendo lenye gharama nafuu na aliwataka kuhakikisha wanalinda mitambo na mashine zilizopo eneo hilo kwani serikali imetumia pesa nyingi katika kuiweka.
Katibu tawala wilaya Ndugu Toba Nguvila akimwakilisha mkuu wa wilaya ndugu Frank Mwaisumbe alipata nafasi ya kumuomba waziri mwenye dhamana ya mawasiliano kuhakikisha huduma ya mawasiliano inakuwa vizuri kwani eneo kubwa la Longido lipo mpakani Zaidi ya kilomita 300. Pia kumuomba waziri kuitengeneza kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka sanya juu wilaya ya Siha mpaka Ngorongoro iliyo chini ya TANROAD kwani ni barabara muhimu ya kupitisha watalii.
Naibu waziri Ndugu Atashasta Justus Nditiye aliwashukuru sana wananchi wa Mundarara kwa kujitokeza kwenye mapokezi yake na kumshukuru mkurugenzi mtendaji wa TTCL kwa kumualika kwenye kuwasha na kuzindua mnara wa mawasiliano na kuwapongeza mhe mbunge,Diwani na ofisi ya mkuu wa wilaya kwa mapokezi makubwa sana.
Mwisho naibu waziri alimalizia kwa kuwataka shirika la TTCL kwa kuhakikisha huduma ya vocha inapatikana na huduma ya internet ya 3G inapatikana katika kata ya mundarara. Pia kuwaahidi wananchi wa Mundarara kuwa serikali itahakikisha inarekebisha barabara kwenye bajeti ijayo na kuhakikisha kuleta minara kwenye baadhi ya kata na vijiji ambavyo mawasiliano sio mazuri.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM