NA ABRAHAM NTAMBARA
SERIKALI ya Wilaya ya Longido imeahidi kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji ya uhakika katika Shule ya Sekondari Natron Flamingo's iliyopo Kijiji cha Meirugoi, Kata ya Gelai Meirugoi, wilayani humo, mkoani Arusha inakwisha ifikapo Januari 2026.
Ahadi hiyo imetolewa Oktoba 13, 2025 na Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Longido Mwl. Gilbert Sombe akizungumza katika Mahafali ya Saba (7) ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo wakati akijibu Risala ya wahitimu, hotuba ya Mwalimu Mkuu sambamba na salamu za Mwenyekiti wa Kijiji cha Meirugoi ambao kwa pamoja walielezea juu ya changamoto hiyo na kumuomba aifikishe katika Vikao vya Halmashauri ili iweze kutatuliwa.
Hata hivyo Mwl. Sombe alikiri Serikali inafahama changamoto hiyo, na kusema kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) wanaendelea kuifanyia kazi na kwamba watahakikisha wanaimaliza haraka.
Kwamba wakati juhudi hizo zikifanyika, Mwl. Sombe aliiagiza Bodi ya Shule hiyo kuitisha vikao haraka iwezekanavyo ili kujadili namna gani wazazi wanaweza kushirikishwa katika kununua Matanki ya Maji ambayo yatatumika kuhifadhia maji ili yawe yanapatikana kwa muda mrefu.
"Kama Serikali tunatambua changamoto hii, hivyo tunaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Maji kumaliza tatizo hili. Hata hivyo naomba Vikao vya Bodi vikae na kutoa maamuzi na sisi tutatekeleza," alisema Mwl. Sombe na kusisitiza,
"Nimatumaini yangu Mwenyekiti na Katibu wa Bodi mtakaa vikao haraka na kuangalia namna kila mzazi atachangia ununuzi wa Matanki. Naomba wazazi mshirikiane kununua Matanki ya Maji ili hata Maji yakiletwa yahifadhiwe, na sisi kama Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji tutahakikisha hadi kufikia Januari mwakani changamoto hii iwe imekwisha,".
Akizungumzia kuhusu Mahafali hayo ya Saba yaliyofanyika shuleni hapo ambayo yalikuwa na jumla ya wahitimu 126 kati ya Wanafunzi 167 walioanza Kidato cha Kwanza mwaka 2022, Mwl. Sombe alisema kutokana na historia ya Shule hiyo kuendelea kupanda kielimu, hategemei kuwepo Mwanafunzi hata mmoja atakayefeli mtihani.
Mwl. Sombe alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao na kwamba wawe wanawatembelea Shuleni badala ya kwenda tu kipindi cha Mahafali, jambo ambalo litawafanya kujua changamoto zinazowakabili na kuweza kushirikia namna ya kuzitatua lengo likiwa ni kuwafanya watoto wasome katika mazingira mazuri.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Hassan Hassan, alisema kuwa wamewaandaa vyema wahitimu hao na kuahidi kuwa watafauli vizuri mtihani wao na kwamba kama Walimu wamefanya sehemu yao na kuwataka wazazi kuendelea kuzungumza na vijana wao kuwaeleza umuhimu wa kusoma na nini jamii inategemea kutoka kwao.
"Vijana hawa tumewanyoosha vya kutosha, hivyo Wazazi sisi kama Walimu tumemaliza kwa nafasi yetu kuwafundisha, kwahiyo na ninyi ni zamu yenu kuwafundisha duniani kuna nini. Mshauri mtoto wako na umueleze nini maana ya kusoma na ajue jamii inategemea nini kutoka kwake," alisema Mwl. Hassan.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.