Na.Happiness Nselu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Wilaya ya Longido kudumisha amani na utulivu, akisisitiza umuhimu wa kushughulikia migogoro iliyopo kwa wakati.
Akizungumza leo katika ukumbi wa J. K. Nyerere wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, CPA Makalla alikutana na watumishi wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wa mila. Alisisitiza kuwa watendaji lazima wafikie wananchi moja kwa moja ili kutatua changamoto na migogoro inayojitokeza.
CPA Makalla alisema kuwa jukumu la viongozi wa serikali na mila ni kushirikiana kuhakikisha mshikamano wa kijamii unadumishwa. “Ni wajibu wetu kuhakikisha wananchi wanashirikiana, migogoro inatatuliwa mapema, na amani inadumishwa kwa maslahi ya maendeleo ya taifa letu,” alisema Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake, Bw. Lekule Laizer, Kiongozi wa Mila, alisisitiza dhamira ya viongozi wa kimila kushirikiana na serikali. “Viongozi wa mila tumejipanga kushirikiana bega kwa bega na serikali kuhakikisha wananchi wetu wanaishi kwa amani, migogoro inatatuliwa mapema, na kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa maslahi ya wilaya na taifa,” alisema Bw. Laizer.
Aidha, CPA Makalla aliongeza kuwa ushirikiano wa karibu baina ya viongozi wa mila, Kamati ya Ulinzi na Usalama na watumishi wa serikali utasaidia kuimarisha mshikamano wa kijamii na kudumisha amani, ambayo ni msingi wa maendeleo na utulivu wa jamii.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.