Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo amewataka Makandarasi na Watumishi wa Umma kufanya kazi kwa weledi na kwa bidii ili kuendana na kasi na malengo ya Serikali ya Awamu ya tano. Mhe Gambo aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido katika Ukumbi wa Halmashauri kwenye Kikao cha kujadili Hoja za Ukaguzi zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo Halmashauri ilipata Hati yenye Mashaka.
Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe Daniel Chongolo akimkaribisha Mkuu wa Mkoa alizungumzia kuibuka kwa Ugonjwa wa Kipindupindu katika Kata ya Gelai Merugoi na kuwa hatua zimechukuliwa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo. Pia alisema hali ya ulinzi na usalama katika Wilaya ni nzuri, hali ya siasa imetulia baada ya Uchaguzi mdogo uliopelekea Dr Kiruswa kushinda Ubunge
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa huduma za kijamii, alisema upatikanaji wa Maji umeongezeka kutoka 21% mwaka 2010 hadi 55% mwaka 2018 na yataongezeka zaidi baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji kutoka Mto Simba. Aliongeza kuwa Mkandarasi mmoja kati ya Wanne wanaotekeleza Mradi huo yuko nyuma kwa utekelezaji na amefikia 17% pekee wakati wenzake watatu wako zaidi ya 90% ya utekelezaji na Wilaya inaomba Serikali ya Mkoa kuingilia kati ili Mkandarasi huyo asiwe kikwazo kwa mradi kukamilika kwa Wakati.
Mhe Chongolo akizungumzia suala la Elimu, alisema Wilaya inakabiliwa na upungufu wa walimu 213 kwa upande wa Shule za Msingi licha ya kuhamisha walimu kutoka Shule za Sekondari kwenda kufundisha Shule za Msingi ndani ya Wilaya. Longido inahitaji msaada kutoka Wilaya ndani ya Mkoa hususan Meru na Monduli zenye ongezeko kubwa la Walimu wa Sekondari ambao wanaweza kufanya kazi kwenye Shule za Msingi Longido.
Kwa upande wa Elimu Sekondari alisema ufaulu umeongezeka kwa Kidato cha Pili na kidato cha Nne Mwaka 2017 lakini ukashuka kwa Kidato cha Sita kutoka 100% Mwaka 2016 hadi 97% Mwaka 2017. Aidha Wilaya imeendelea kupokea fedha za P4R ambapo Mwaka 2018 imepokea Tshs 438,113,802.67
Kuhusu Utawala na Utumishi, Mkuu wa Wilaya alifafanua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido ina Wakuu wa Idara Watano na Wakuu wa Vitengo Wanne wanaokaimu kwa muda mrefu na kuwafanya kukosa kujiamini katika kufanya maamuzi, pia ina changamoto zinazotokana na Watumishi wengi kuhama ikiwemo walimu na Watumishi wa Kada za Afya na maombi ya Uhamisho yamekuwa yakiongezeka. kuruhusiwa kuhama kwa Watumishi kunaathiri Ikama.
Aidha alisema kuwa Longido haina Hospitali ya Wilaya, lakini tayari Serikali imetoa zaidi ya Bilioni moja kwa ajili ya kuimarisha utoaji nwa huduma za Afya kwa kufanya Ujenzi wa Kituo cha Afya Eorendeke kilichopo katika mpaka wa Tanzania na Kenya, na kuboresha Kituo cha Afya cha Engarenaibor na shughuli za Ujenzi zinaendelea. Pia aliwasilisha ombi la Wilaya kwa Mkoa kusaidia kufuatilia Tshs Milioni 800 zilizosomeka kwenye Mfumo kuwa zimetumwa Wilaya ya Longido kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya lakini Fedha hizo hazijaingia kwenye Akaunti za Halmashauri kama ilivyo katika maeneo mengine yaliyopata fedha hizo.
Mhe Chongolo akizungumzia Maendeleo ya Sekta ya Mifugo alisema upatikanaji wa Malisho na Afya za Mifugo umeimarika kufuatia Mvua zilizonyesha ndani ya Wilaya. Aidha Wilaya ilivuka lengo la upigaji Chapa Mifugo kwa kupiga Chapa Mifugo kwa 110%
Kuhusu Kilimo alisema 64% ya Chakula kinatoka nje ya Wilaya na katika kuimarisha uhifadhi na uparikanaji wa Chakula, maghala mawili ya mfano yamejengwa katika Kata ya Engarenaibor na Sinya chini ya Miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na yana uwezo wa kuhifadhi tani 900 kila moja. Pia uhamasishaji wa uhifadhi wa Chakula umefanyika ambapo magunia zaidi ya 6,000 yamehifadhiwa na hakuna upungufu wa Chakula kwa sasa.
Kadhalika akielezea hali ya Miundombinu ya Barabara za Wilaya alisema Barabara nyingi zimeharibiwa na mvua iliyonyesha na licha ya changamoto hiyo kuna matumaini kuwa zitakarabatiwa kwa Mwaka wa fedha 2018/2019 baada ya TARURA Wilaya ya Longido kuongezewa fedha kwenye bajeti yao. Aidha alisema Wilaya inashauri kuwe na mfumo wa kuhifadhi fedha za dharura katika Ofisi za TARURA Mkoa ambazo zitasaidia kufanya matengenezo ya dharura ya Miundombinu ya barabara pale zinapoharibika wakati wa mvua na kusababisha kukatika kwa mawasiliano.
Katika Sekta ya Ardhi na Maliasili, Mhe Chongolo alisema Wilaya inakabiliwa na changamoto ambapo baadhi ya wawekezaji kwenye vitalu vya Uwindaji hawafanyi doria za uhifadhi kama inavyohitajika kwa mujibu wa Miongozo na kuongeza kuwa hali hiyo itaisha endapo mchakato wa kuanzisha WMA ya ziwa Natron utakamilika na kurudisha umiliki kwa wananchi ambao ni sehemu muhimu ya uhifadhi, hivyo akatoa wito kwa Wizara ya Utalii na Maliasili kulitazama suala hilo na kulipa msukumo unaostahili.
Mbunge wa Jimbo la Longido Mhe Dr Stephen Kiruswa kwa upande wake aliishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa Magari kwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi. Magari hayo matatu – Double Cabin ni kwa ajili ya Chanjo, Suzuki Maruti ni Gari la Wagonjwa na Toyota landcruiser pick up kwa ajili ya Sekta ya Maliasili.
Mkuu wa Mkoa akizungumzia mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu alisema ugonjwa huo unaosababishwa na uchafu ni aibu kwa Wilaya na akaelekeza Watendaji wa Vijiji, Kata, Tarafa, na Maafisa Afya katika maeneo yenye Ugonjwa huo kumpa Taarifa za idadi za Kaya ambazo zina vyoo na ambazo hazina Vyoo pamoja na hatua zilizochukuliwa kwa kaya ambazo hazina vyoo. Pia alisema Watendaji hao maeneo yao yakithibitika hayana vyoo kila Kaya ipewe miezi mitatu kujenga vyoo na Mikataba iandikishwe baina ya Maafisa Afya na Kaya hizo kuhusu Ujenzi wa vyoo ndani ya miezi mitatu kuanzia tarehe 14/05/2018. Aidha alihimiza kuboreshwa kwa hali ya Vyoo kwenye Shule na kuongeza kuwa kuna haja ya kuanzisha Kampeni Maalum ya kujenga Vyoo ndani ya Mkoa wa Arusha ili kukabiliana na Magonjwa kama hayo.
Kuhusu hoja za Ukaguzi za Mwaka ulioishia Juni 2017, Mhe Gambo alisema baadhi ya Watendaji wa Halmashauri hawajaifahamu filosofia ya Rais Magufuli ya kufanya kazi hivyo akawataka Watumishi kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na kwa maslahi ya wananchi na wale watakaoshindwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maji na maelekezo ya Mhe Rais katika sekta za Maji na Ardhi, alisema Serikali imewekeza kwenye kuhakikisha Wananchi wanapata maji safi na salama kwa kutenga fedha za utekelezaji wa miradi ya Maji na Serikali ya Mkoa haitakuwa tayari kuona Wataalam na Makandarasi wachache wanasababisha kutofikiwa kwa lengo hilo la Serikali. Alisema Mkoa utashirikiana na Wilaya pamoja na Wizara kufikia lengo ikibidi kuwaondoa makandarasi wasio na uwezo. Pamoja na hayo alisema kuna changamoto kwenye usimamizi wa baadhi ya miradi ya Maendeleo ambapo awali walitumika makandarasi lakini kutokana na madhara ya 10% miradi haikufikia malengo na kuanzia sasa itatekelezwa kwa force account ambayo imekuwa ikipigwa vita kwa sababu hakuna tena 10% licha ya miradi hiyo kuwa na tija kubwa. Alisema utaratibu huo ni mzuri na kila inapowezekana force account itumike kwa kufuata taratibu isipokuwa kwa miradi mikubwa zaidi.
Akizungumzia Mpango wa Elimu wa Mkoa, Mhe Gambo alisema Elimu ni kipaumbele cha kwanza cha mkoa ili kupandisha kiwango cha Elimu kwa 50% na kuongeza kuwa yapo makubaliano yaliyowekwa katika kila ngazi yakihusisha Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu, Wakaguzi wa Ubora, Waratibu wa Elimu Kata ambayo yanasisitiza utekelezaji na usimamiaji wa mgawanyo wa majukumu. Ili kufikia azma hiyo, kuanzia Mwaka 2018 Mkoa umeanzisha Mtihani wa pamoja wa Mkoa kuanzia Shule za Msingi na Sekondari ambao utafanyika kila mwishoni wa Muhula na umewekewa utaratibu ili kuboresha Elimu badala ya kuangalia matokeo pekee
Mhe Gambo akizungumzia Hoja za Ukaguzi alisema Longido imepata Hati ya mashaka kwa miaka minne mfululizo na Hoja nyingi zimechangiwa na uzembe hivyo hatua sharti zichukuliwe kwa wote waliosababisha au kuhusika kutokea kwa Hoja hizo. Hoja hizo ni pamoja na kutoonekana kwa Vitabu 22 vya kukusanyia mapato, Malipo yasiyo na Viambatanisho, Malipo ya Mishahara kwa Watumishi waliofariki, Malipo yaliyolipwa zaidi kwa Waheshimiwa Madiwani na Watumishi kinyume na Miongozo, na Malipo yasiyo na manufaa kwa Halmashauri. Pamoja na hoja hizo Halmashauri ina Hoja 91 za Mwaka 2016/2017 na Hoja 102 za miaka ya nyuma ambazo bado utekelezaji wake haujahakikiwa na CAG. Maelekezo ya Jumla yaliyotolewa ni pamoja na Katibu Tawala Mkoa (RAS) kuchukua hatua kwa kuhakikisha Afisa Utumishi anayehusika na Mfumo wa lawson, na Mkuu wa Idara ya Utawala & Utumishi wa wakati huo wanachukuliwa hatua kwa kuwa wanawajibika moja kwa moja kusimamia na kuidhinisha malipo ya Mishahara ambayo ililipwa kwa Watumishi ambao hawakuwa kazini. Pia alielekeza Halmashauri ionyeshe hatua zitakazochukuliwa per Sheria, Kanuni na Taratibu kwa Wahusika.
Kuhusu Upungufu wa Nyaraka (Vitabu vya mapato), alielekeza Mhasibu anayesimamia eneo la Pre audit aondolewe kwenye nafasi hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuhakiki nyaraka zote za malipo.
Pia kuhusu Malipo yasiyo na viambatanisho alielekeza Watumishi wote ambao walipaswa kuandaa na kuwasilisha viambatanisho hivyo wachukuliwe hatua ka kushindwa kuviwasilisha wakati wa ukaguzi, lakini pia Watumishi wote wanaodaiwa masurufu wakatwe kwenye mishahara yao, walipe faini kwa kuchelewa kurudisha masurufu hayo, na waandikiwe barua za onyo.
Kuhusu Fedha za Mahindi ya Njaa, alielekeza RAS kuandaa orodha ya wote waliosababisha Hoja hiyo na hatua stahili zitachukuliwa kuanzia ngazi ya Kitongoji hadi Halmashauri.
Pia alielekeza kuimarishwa kwa usimamizi ili Fedha za 10% za Vijana na Wanawake ziweze kutolewa kwa Vikundi kila mwezi kwa mujibu wa taratibu
Kadhalika alielekeza Fedha zilizotumwa kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania kama Kodi na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutokana na Mishahara iliyolipwa kwa Watumishi ambao hawakuwa kazini zifuatiliwe na kurudishwa Hazina.
Kadhalika aliagiza Watumishi wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kusababisha Hoja za Ukaguzi waandikiwe barua za Onyo ikiwemo Wajumbe wote wa Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa kushindwa kuchukua hatua mapema.
Aidha alielekeza Waheshimiwa Madiwani na Watumishi waliolipwa Posho zaidi ya walivyopaswa kulipwa kwamujibu wa Miongozo ya Serikali warudishe fedha hizo kabla ya tarehe 30 Juni, 2018
Pamoja na hayo alitoa maelekezo kwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia hoja iliyotokana na mapato ya Tshs 149,096,920 yaliyokusanywa na Mawakala bila kuwa na Mikataba pamoja na matumizi ya Vitabu vya Mawakala kuwa na namba za stakabadhi zinazofanana katika ukusanyaji wa mapato
Pia alielekeza inapowezekana Ofisi ya CAG iwe inahusishwa kwenye michakato ya kuelekea kwenye utoaji wa Zabuni mbalimbali ili kuepusha kutokea kwa makosa yanayoweza kuepukika.
Mhe Gambo akihitimisha Kikao hicho alielekeza Majibu ya awali ya Hoja zote za Ukaguzi yawasilishwe Ofisi za Ukaguzi (NAO) kufikia tarehe 18 Mei 2018.
Mkuu wa Mkoa na ujumbe wake wataendelea na ziara katika Wilaya ya Longido itakayohitimishwa tarehe 16/05/2018 ambapo atafanya Mkutano wa hadhara Mundarara, atakagua miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ikiwemo Ujenzi wa Vituo vya Afya cha Eorendeke, Engarenaibor, Ketumbeine, Madarasa, Maabara, na Mradi wa Maji kutoka chanzo cha Mto Simba.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM