Serikali wilayani Longido imewahakikishia wafanyakazi kuwa serikali sikivu ya awamu ya tano itahakikisha uunganishwaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii unalenga kuboresha mafao ya wafanyakazi na si vingenevyo.
Ahadi hiyo ya serikali imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya longido Daniel G.Chongolo alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) iliyofanyika kiwilaya mjini Longido.
Chongolo ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amesema serikali chini ya uongozi imara wa Rais John Pombe Magufuli ilifanya uamuzi wa kutunga sheria ya uunganishaji wa mifuko hiyo ya hifadhi za jamii kwa lengo la kuongeza tija ya mafao kwa watumishi na kuepusha urasimu usiokuwa na tija.
Aidha akijibu hoja zilizotolewa na wafanyakazi kupitia risala yao, Mkuu huyo wa wilaya ya Longido amesisitiza kuwa serikali inatambua changamoto nyingi zinazowakumba wafanyakazi wake, zikiwemo za kupandishwa vyeo, madai ya malimbikizo ya madeni, uhaba wa nyumba za watumishi pamoja na changamoto za mazingira magumu ya kazi na kuwahakikishia kuwa serikali inazifanyia kazi changamoto zote ili kuwafanya watumishi wabakize wajibu wa kutenda kazi pekee.
Changamoto ambazo zimeanza kutatuliwa ni pamoja na kulipwa kwa madeni ya watumishi zoezi lililoanza mwezi Machi 2018, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi katika maeneo ya pembezoni, pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa ujumla.
Kwa upande wake Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Longido Mikidadi Ally amewakumbusha waajiri wa serikali na sekta binafsi kuwa kisheria chini ya kifungu cha 31 cha matumizi mabaya ya madaraka ni kosa la jinai kutokupeleka michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii.
Maandimisho ya Mei Mosi mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo "Uunganishwaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ulenge kuboresha mafao ya wafanyakazi".
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM