Na Happiness Nselu
Longido, 22 Janauri 2025 – Watoto wanaoishi katika kituo cha nyumba salama Wilayani Longido wamenufaika na msaada wa sadaka kutoka kwa viongozi wa dini na wananchi,Sadaka hizo zimewasilishwa na viongozi hao walipowatembelea watoto hao katika kituo hicho cha nyumba salama kilichopo wilayani humo mnamo tarehe 21.01.2025. Sadaka zilizowasilishwa zilitolewa wakati wa dua ya kuiombea wilaya na taifa iliyofanyika tarehe 28.12.2024,Dua iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Salumu Kalli.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Viongozi wa Dini wa Wilaya ya Longido, Shekhe Ramadhani Mpangala, alikabidhi sadaka hizo kwa niaba ya wananchi wa wilaya. Shekhe Mpangala alisisitiza umuhimu wa kujitolea na mshikamano kwa ajili ya watoto wanaoishi katika nyumba salama, ambao wanahitaji msaada wa kila aina ili kukabiliana na changamoto za maisha. Alisema msaada huo ni muhimu katika kuhakikisha watoto hao wanapata mahitaji ya msingi ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza na kuimarisha maisha yao.
Mchungaji Aidan Mwikolla, ambaye pia alizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini, aliwataka wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kutoa msaada kwa watoto hao. Alieleza kuwa msaada huo unajumuisha vitu muhimu kama nguo, chakula, madaftari, na vifaa vya shule, ambavyo vitasaidia watoto hao kuendeleza masomo yao na kuwa na maisha bora. Aliongeza kuwa kutoa sadaka kwa watoto hawa ni jukumu la kila mmoja katika jamii, kwani watoto ni hazina ya taifa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Longido na Kamati ya Usimamizi wa Nyumba Salama, Bw. Omary Ramadhani, alitoa shukrani kwa viongozi wa dini na wananchi waliotoa sadaka zao. Alisema kuwa msaada huo ni muhimu hasa kwa watoto wanaoishi katika nyumba salama, ambapo wengi wao wanategemea msaada wa jamii kwa ajili ya kuendelea na masomo na maisha yao ya kila siku. Aliwashukuru wananchi kwa kujitolea na kuwataka kuendelea kuwasaidia watoto hawa ili waweze kupata mahitaji yao ya msingi, kwani wapo wanafunzi wengi ambao wanategemea msaada huu ili kuweza kufanikiwa katika masomo yao.
Afisa Ustawi wa Wilaya, Bw. Abdalah Nyange, ambaye alikabidhi msaada kwa niaba ya watoto, alitoa shukrani kwa viongozi wa dini, ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya, na wananchi kwa msaada wao endelevu. Bw. Nyange alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidia watoto hawa, huku akisisitiza kuwa bado mahitaji ni makubwa. Alitoa wito pia kwa jamii kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kuhakikisha familia zinazingatia malezi bora ya watoto kwa upendo. Aliitaka jamii kuwa na moyo wa huruma na kutoa msaada bila kutarajia malipo ili kuleta mabadiliko chanya kwa watoto hao.
Hafla hiyo ilionyesha mshikamano wa kipekee wa wananchi wa Longido katika kusaidia watoto wanaoishi nyumba salama, huku viongozi wa dini na wadau mbalimbali wakitumia fursa hiyo kutoa wito wa kuendeleza msaada kwa watoto hao na kuhakikisha wanapata maisha bora na ya kimaendeleo. Viongozi hao walisisitiza kuwa msaada wa jamii ni muhimu ili watoto hawa waweze kufikia ndoto zao na kuwa raia bora wa taifa la kesho.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM