Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori imetoa malipo ya kifuta Machozi/Jasho cha Tsh. 4,200,000 kwa wakazi 13 wa Wilaya ya Longido waliojeruhiwa/kuumizwa na wengine kuuawa kwa kushambuliwa na wanyamapori hatari/wakali wakiwa katika shughuli zao za kila siku za hapa na pale mwaka 2018 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Longido.
Wakitoa kifuta Machozi/Jasho leo Mei 13, 2019 wawakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mkoani Arusha kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Arusha, ndugu Martina Kalunde (Afisa Wanyamapori) na John Msangi (Mhasibu) mbele ya Afisa Wanyamapori Wilaya ya Longido ndugu Lomayani Saiguran Lukumay kwa wakazi 13 waliomba kuwepo na uthibitisho kutoka kwa watendaji wa Vijiji kuwa wahusika waliyofika mbele yao kwa ajili ya malipo ndio wahusika halali wa matukio hayo ya kujeruhiwa/kuuawa na wanyamapori hatari/wakali.
Martina Kalunde (Afisa Wanyamapori kutoka TAWA) amefafanua kuwa wakazi waliopewa kifuta Machozi/Jasho ni wale waliotambuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji (W) na kujaziwa fomu ya Kifuta Machozi/jasho na kutumwa kwa Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori Dodoma kuomba malipo kwa wahanga. Baada ya fomu hizo kufika Dodoma Wizara ilimwagiza Mkururgenzi Idara ya Wanyamapori kufanya uhakiki wa madai hayo kwa kufika kwenye Wilaya husika. Kwa Wilaya yetu Uhakiki wa Wizara ilifanyika mwezi wa pili 2019 na kubaini wananchi 11 waliojeruhiwa majeraha ya muda na 02 kuuawa na wanyamapori hatari/wakali. Matukio haya yaliwahusisha wanyamapori aina ya Tembo, Nyati, Simba na Fisi.
Afisa huyo aliendelea kwa kutoa ufafanuzi juu ya malipo hayo na kusema kwamba, kwa mujibu wa Kanuni ya Kifuta Machozi/Jasho ya mwaka 2011, mtu akiuawa na mnyamapori hatari atalipwa kiasi cha shilingi za Kitanzania 1,000,000 kama Kifuta Machozi, 500,000 kama amepata ulemavu wa kudumu na 200,000 kama ni mjeraha ya kupona baada ya muda. Aidha aliorodhesha kwa kuwataja aina wanyamapori waliotajwa kisheria kwa Malipo ya Kifuta Machozi/Jasho na kusema kuwa ni Simba, Nyati, Fisi, Kiboko, Faru, Tembo na Mamba.
Kwa upande wake Afisa Wanyamapori Wilaya ya Longido Lomayani Saiguran Lukumay amebainisha kuwa kifuta Machozi/Jasho hiki kwa wahanga wa wanyamapori Hatari/wakali ni ishara tosha kuwa serikali iko pamoja na wananchi wake kwa kujali haki na thamani yao. Aidha aliishukuru serikali kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji (W) kwa malipo hayo kwa wananchi waliojeruhiwa/kuuawa na wanyamapori huku akisema kwamba malipo hayo yatasaidia kuendeleza uvumilivu wa wananchi kuishi na wanyamapori katika maeneo yao kwa amani.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: 027-2539603
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved. Designed by Loth Zacharia & Joseph Peter Mkumbwa Sponsored by GWF TAMISEM